Ruto awapongeza washindi wa uchaguzi

DP amewapongeza hasa wanawake walioshinda nafasi za kuchaguliwa.

Muhtasari

•Mgombea urais wa huyo wa chama cha UDA amewapongeza hasa wanawake walioshinda nafasi kubwa za kuchaguliwa.

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: Facebook//WilliamSamoeiRuto

Naibu rais William Ruto amewapongeza washindi wote wa uchaguzi uliofanyika siku ya Jumanne, Agosti 9.

Mgombea urais wa huyo wa chama cha UDA amewapongeza hasa wanawake walioshinda nafasi kubwa za kuchaguliwa.

"Hongera kwa washindi wote wa uchaguzi. Hasa, tunasherehekea wanawake wengi ambao wamevunja vizuizi vya kupanda ngazi ya kisiasa," Ruto alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Haya yanajiri huku shughuli ya kutangazwa kwa washindi wa viti mbalimbali na kuwatunuku vyeti ikiendelea kote nchini.

Ruto amewatakia kheri njema viongozi wote waliochaguliwa huku wakisubiri kuanza kazi mpya walizokabidhiwa.

"Kila la heri mnapoanza majukumu yenu mapya. Hustlers wanawategemea," Alisema.

Tume ya IEBC tayari imewatangaza washindi kadhaa wa viti vya ugavana, ubunge, useneta, uwakilishi wa wanawake na hata wajumbe wa kaunti.

Hata hivyo mshindi wa kiti cha urais bado hajatangazwa huku naibu rais na mgombea wa Azimio Raila Odinga wakipatiana ushindani mkubwa katika matokeo yaliyotangazwa tayari kutoka maeneobunge mbalimbali.