Waangalizi wa EAC walivyoridhishwa na mchakato wa kura Kenya

Waangalizi wameipongeza IEBC Kwa jinsi ilivyotekeleza zoezi la upigaji kura Jumanne.

Muhtasari

•Waangalizi walisema kwamba polisi walikuwa katika nafasi ya kuhakikisha wapiga kura wanalindwa wakati wa zoezi hilo katika vituo vya kupigia kura.

Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete
Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Kikwete
Image: BBC

Ujumbe wa Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nchini Kenya umeipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kutekeleza zoezi la upigaji kura lililokamilika Jumanne.

Katika hotuba kwa wanahabari Alhamisi jijini Nairobi, ujumbe wa waangalizi ulisema kwamba polisi pia walikuwa katika nafasi ya kuhakikisha wapiga kura wanalindwa wakati wa zoezi hilo katika vituo vya kupigia kura.

Kiongozi wa ujumbe huo Jakaya Kikwete (Rais wa zamani wa Tanzania) alisema kuwa polisi hawakuingilia zoezi la upigaji kura.

‘”Ujumbe unaipongeza IEBC kwa kutumia vyema teknolojia katika usajili wa wapigakura, kuwatambua wapigakura na uwasilishaji wa matokeo,” Bw Kikwete alisema.

Alisema teknolojia hiyo imeongeza ufanisi na kuongeza uwazi nchini, tofauti na chaguzi zilizopita.

Hata hivyo, Bw Kikwetre alisema kulikuwa na matukio machache yanayohusiana na utambulisho wa wapigakura na kitengo cha KIEMS, akiomba tume kuzingatia masuala hayo na kutatua siku zijazo.

"Tunapendekeza kwamba matatizo yanayohusiana na vifaa vya KIEMS yatambuliwe na hatua muhimu za kurekebisha zichukuliwe kwa utendakazi bora katika siku zijazo."