Tuna imani kuwa tutashinda uchaguzi, Wajackoyah asema

Wajackoyah alisema ikiwa mchakato huo ni wa haki, huru na wa kuaminika, watajinyakulia mamlaka.

Muhtasari
  • Hata hivyo, Mwaure alikubali kushindwa na kumuunga  mgombea urais wa UDA William Ruto
Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Image: The star

Mgombea urais wa chama cha Roots George Wajackoyah amesema wana imani kwamba watashinda uchaguzi ambao umekamilika hivi punde.

Kupitia taarifa, Wajackoyah alisema ikiwa mchakato huo ni wa haki, huru na wa kuaminika, watajinyakulia mamlaka.

“Kama mnavyofahamu, mgombea wetu wa urais ni mmoja kati ya Wakenya wanne wanaosaka afisi ya juu zaidi nchini ili kubadilisha nchi yetu na kuifanya Kenya kuwa gwiji la mwanauchumi,” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.

Wajackoyah alisema atahutubia taifa baada ya rais kutangazwa.

"Wananchi walitekeleza awamu ya kwanza, na awamu ya pili na IEBC, chombo hicho kikatiba kiliidhinisha kujumlisha kura na kumtangaza mshindi. Mgombea wetu atahutubia taifa baada ya kutangazwa rasmi na IEBC," akasema.

Kinyang'anyiro cha urais kilikuwa kimewavutia wagombeaji wanne; Kiongozi wa chama cha UDA William Ruto, Raila Odinga wa Azimio, na kiongozi wa chama cha Agano Waihiga Mwaure.

Hata hivyo, Mwaure alikubali kushindwa na kumuunga  mgombea urais wa UDA William Ruto.

Mwaure alisema ameona takwimu zilizoonyeshwa na IEBC zinamuunga mkono Ruto na alikuwa anakubaliana na manifesto ya UDA.

"Baada ya mazungumzo ya kina na timu zetu huko Bomas, tumekuwa tukifuata utaratibu unaoendelea na kuashiria kuwa takwimu ziko na bila shaka zimekuwa zikimuunga mkono William Ruto," alisema.