Mitambo ya IEBC ilidukuliwa- WanaAzimio wadai

Kanchory alidai kuwa mifumo ya tume hiyo ilidukuliwa wakati shughuli ya uhakiki wa kura ulipokuwa unaendelea.

Muhtasari

•Ajenti mkuu wa Raila Odinga Saitabao Ole Kanchory alisema matokeo yaliyojumuishwa na IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya hayakuweza kuthibitishwa.

Saitabao Kanchori akiandamana katika kituo cha kitaifa cha kuhesabu kura cha IEBC cha Bomas mnamo Agosti 14,2022
Saitabao Kanchori akiandamana katika kituo cha kitaifa cha kuhesabu kura cha IEBC cha Bomas mnamo Agosti 14,2022
Image: MAKTABA

Timu ya Azimio-One Kenya sasa inadai kuwa tume ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) haikuendesha uchaguzi wa mwaka huu kwa uwazi.

Akihutubia waandishi wa habari Jumatatu jioni, Ajenti mkuu wa Raila Odinga Saitabao Ole Kanchory alisema matokeo yaliyojumuishwa na IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya hayakuweza kuthibitishwa.

Kanchory aliibua madai kuwa mifumo ya tume hiyo ilidukuliwa wakati shughuli ya uhakiki na ujumuishaji wa kura ulipokuwa unaendelea.

"Tuna taarifa za kijasusi kuwa mfumo wao ulipenyezwa na kudukuliwa na kwamba baadhi ya maafisa wa IEBC walitenda makosa ya uchaguzi na baadhi yao wanapaswa kukamatwa ikiwa hawajakamatwa," Kanchory alisema.

Ajenti huyo udukuzi wa mitambo ambao alidai ulikuwa unaendelea katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura ndio ulifanya aseme kuwa "Bomas ni eneo la uhalifu."

Alibainisha kuwa IEBC ilipaswa kutoa matokeo ambayo yanaweza kuliongeza kuwa hawajaweza kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa urais.

“Matokeo ambayo hayawezi kuthibitishwa si matokeo na mwenyekiti (Wafula Chebukati) alikuwa amewahakikishia Wakenya kuwa ataendesha uchaguzi huu kwa uwazi jambo ambalo hajafanya,” Kanchori aliongeza.