Sababu zinazoweza kumfanya Rais Uhuru Kenyatta kuhudumu zaidi ya muhula wake

Kumekuwa na madai kwamba kiongozi huyo alikuwa anapanga kuhudumu zaidi ya muhula wake aliopatiwa na katiba.

Muhtasari

•Kura iliyopigwa tarehe 9 Agosti mwaka huu imekuwa ya ushindani mkali zaidi katika historia ya taifa hili hususan wakati ambapo rais aliyepo madarakani anaondoka.

•Kwa mujibu wa Ibara ya 142(1) ya Katiba, "Rais atachukua madaraka kwa muhula unaoanzia tarehe ambayo Rais aliapishwa, na kumalizika rais mpya atakapoapishwa 136 (2) (a). ) ''.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Uchaguzi wa Kenya siku zote huwa na ushindani mkali lakini kura iliyopigwa tarehe 9 Agosti mwaka huu imekuwa ya ushindani mkali zaidi katika historia ya taifa hili hususan wakati ambapo rais aliyepo madarakani anaondoka.

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, amekuwa akizozana na Naibu wake William Ruto, ambaye alichangia pakubwa ushindi wake katika chaguzi mbili zilizopita.

Badala ya kumuunga mkono Ruto kama alivyokuwa ameahidi hapo awali, Kenyatta ameweka uzito wake nyuma ya kinara mkongwe wa upinzani Raila Odinga, ambaye akiwa na umri wa miaka 77 anashiriki kwa mara ya tano na huenda ikawa mara yake ya mwisho kupigania wadhfa huo.

Vile vile mbali na Ruto na Raila kuna wagombea wengine wawili waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho nao ni George Wajackoya na Waiga Mwaure.

Ijapokuwa wagombea hao wote wanaweza kuingia madarakani mapema Septemba, iwapo Wakenya watamuingiza mmoja wao Ikulu, kuna matukio ambayo yanaweza kusababisha nchi kusubiri hadi mwaka ujao kwa Rais wa 5 kuapishwa, hatua ambayo itaongeza muda wa rais aliyepo madarakani kuhudumu hadi rais mpya atakapopatikana.

Kwa mujibu wa Ibara ya 142(1) ya Katiba, "Rais atachukua madaraka kwa muhula unaoanzia tarehe ambayo Rais aliapishwa, na kumalizika rais mpya atakapoapishwa 136 (2) (a). ) ''.

Tayari rais Kenyatta amewaondoa hofu Wakenya kuhusu iwapo ataongeza muhula wake zaidi ya miaka 10, na kuwahakikishia kwamba uchaguzi wa kumchagua mrithi wake utafanyika tarehe 9 Agosti 2022 kama ilivyo.

Hatua hii inajiri huku kukiwa na madai kutoka kwa wakosoaji wake kwamba kiongozi huyo alikuwa anapanga kuhudumu zaidi ya muhula wake aliopatiwa na katiba

Lakini Je ni matukio gani yanayoweza kumuongezea muda rais Uhuru Kenyatta kuhudumu kikatiba?

Iwapo kesi ya kupinga matokeo itawasilishwa mahakamani

Kifungu cha 136 kinaeleza uchaguzi wa urais utafanyika Jumanne ya pili ya Agosti, katika kila mwaka wa tano. Kifungu cha 140 cha Katiba hata hivyo kinatoa nafasi kwa maswali kuhusu uhalali wa uchaguzi wa urais katika Mahakama ya Juu Zaidi.

Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?

Ombi la kupinga matokeo hayo linaweza kuwasilishwa katika Mahakama ya Juu ndani ya siku saba baada ya kutangazwa kwa matokeo na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka. Ikiwa matokeo ya mwisho yatatangazwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC) ndani ya siku 7 zilizowekwa na Katiba kwa uchaguzi wa wiki ijayo, basi malalamiko yanaweza kuwasilishwa hadi Agosti 23.

Kwa hali ya kawaida iwapo hakuna ombi lililowasilishwa kufikia Agosti 23, basi rais mpya ataapishwa Agosti 30, ambayo ni siku 14 baada ya siku ya mwisho ambayo IEBC inaweza kutangaza matokeo ya urais na kwa mujibu wa Kifungu 141(2)(a) cha Katiba ya 2010.

Mahakama ya Juu, kwa mujibu wa katiba, nayo itakuwa na siku 14 kubainisha maombi ya kupinga uhalali wa uchaguzi wa urais. Hii itachukua muda wa kuapishwa kwa rais mpya hadi Septemba 13, ikiwa maombi yaliyowasilishwa mwezi Agosti yatatupiliwa mbali na Mahakama ya Juu kama ilivyofanyika mwaka wa 2013.

Iwapo uchaguzi utabatilishwa katika Mahakama ya Juu kama ilivyokuwa mwaka wa 2017, uchaguzi mpya utafanywa kuanzia Novemba 6 - siku 60 baada ya kutolewa kwa uamuzi kulingana na Kifungu cha 140(3) - huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa ndani ya siku 7. Ikiwa uchaguzi mpya utatangazwa mnamo Novemba 13, rais mpya ataapishwa ifikapo Novemba 27 ikiwa hakutakuwa na ombi lililowasilishwa ifikapo Novemba 20.

Ikiwa matokeo mapya yatapingwa, basi Mahakama ya Juu itapitia mchakato wa awali na rais mpya ataapishwa kufikia Desemba 11 ikiwa uamuzi utafanywa kuwa matokeo ya uchaguzi ni halali.

Iwapo Mahakama ya Juu itabatilisha matokeo mapya ya uchaguzi, Wakenya watalazimika kurejea kwenye upigaji kura Februari 4, 2023, matokeo yakitarajiwa kutolewa haraka zaidi Februari 11, 2023. Ikiwa hakuna ombi lililowasilishwa kufikia Februari 18, basi matokeo mapya yanatarajiwa. Rais ataapishwa ifikapo Februari 25.

Iwapo ombi litawasilishwa kufikia Februari 18, 2023, na kutupiliwa mbali na Mahakama ya Juu kufikia Machi 4, 2023, rais mpya ataapishwa kufikia Machi 11, 2023.

Hakuna kikomo katika Katiba kuhusu muda gani mzunguko huu unaweza kuendelea, na wakati wote huo rais aliyepo madarakani ataendelea kuhudumu hadi pale rais mpya atakapopatikana.

Awamu ya pili ya Uchaguzi

Katika uchaguzi wa urais wa Kenya, mgombea hutangazwa kuwa rais ikiwa amepokea zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi (asilimia 50 pamoja na moja); na angalau asilimia ishirini na tano ya kura zilizopigwa katika kila zaidi ya nusu ya kaunti.

Iwapo hakuna mgombea anayetimiza kizingiti hiki , uchaguzi wa marudio utafanyika ndani ya siku thelathini baada ya uchaguzi uliopita. Kwa usahihi zaidi, matokeo yatarudiwa katika mojawapo ya hali zifuatazo: ambapo mgombea anayeongoza atapokea 50% pamoja na kura moja iliyopigwa lakini hajapata 25% ya kura zilizopigwa kwa zaidi ya nusu ya kaunti zote, iwapo mgombeaji atapata 25% ya kura zilizopigwa katika zaidi ya nusu ya kaunti lakini hajapata 50% pamoja na kura moja iliyopigwa; au iwapo hakuna mgombea anayepokea 50% pamoja na moja kati ya jumla ya kura zilizopigwa wala 25% ya kura zilizopigwa katika zaidi ya nusu ya kaunti nchini.

katika tukio hili duru ya pili itafanyika kati ya mgombea au wagombea waliopata idadi kubwa zaidi ya kura. Muda ambao mchakato huu wote unahitajika kufanyika ni ndani ya siku 30. Katika kipindi chote cha marudio ya uchaguzi , rais aliyepo madarakani ataendelea kuhudumu hadi rais mpya atakapotangazwa na kuapishwa.

Iwapo mgombea mmoja wa urais atafariki kabla ya uchaguzi

Wakati kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais kinapopamba moto, kifo cha mmoja kati ya wagombea wanne wa urais - hali ambayo hakuna mtu angetamani itokee - kinaweza kutokea.

Katiba ya 2010, kwa kutambua uwezekano huo, imeorodhesha katika Ibara ya 38(8)(b) kifo cha mgombea wa kuchaguliwa kuwa Rais au Naibu Rais kabla ya tarehe ya uchaguzi iliyopangwa kuwa mojawapo ya sababu zitakazopelekea kufutwa kwa uchaguzi wa urais. Punde tu uchaguzi utakapofutwa , Uchaguzi mpya utalazimika kufanyika katika kipindi cha siku 60 baada ya tarehe ya uchaguzi wa awali kulingana na katiba.

Hali kadhalika uchaguzi unaweza kuahirishwa iwapo kuna janga lililotokea kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Wakati huu wote rais aliyepo madarakani ataendelea kuhudumu hadi uchaguzi mpya utakapofanyika na rais mpya kutangazwa na kuapishwa.