Wasiwasi nchini huku raia wakingoja tume ya IEBC kumtangaza rais mpya

Hamu ya wengi imeelekezwa katika ukumbi wa Bomas ambako kura za urais zimekuwa zikijumlishwa.

Muhtasari

•Tangu wapiga kura kupanga foleni jumanne iliyopita na kuwachagua viongozi wao-matokeo ya nafasi nyingine tano yameshatolewa .

•Biashara nyingi hazijafunguliwa na wengi watangoja tangazo la IEBC kabla ya hali ya kawaida kurejea katika mji huo .

Image: BBC

Kimekuwa kipindi cha takriban siku sita za kungoja matokeo ya kura ya urais nchini Kenya .Tangu wapiga kura kupanga foleni jumanne iliyopita na kuwachagua viongozi wao-matokeo ya nafasi nyingine tano yameshatolewa .

Hata hivyo hamu ya wengi imekuwa ikielekezwa katika ukumbi wa Bomas ambako kura za urais zimekuwa zikijumlishwa na matokeo ya maeneo mbalimbali kutangazwa .

Leo Jumatatu kwa kawaida huwa siku ya shughuli nyingi katika Maisha ya kila siku ya raia-lakini sio Jumatatu hii.Wengi wanafanyia kazi nyumbani na kuna baadhi ya wafanyabiashara hawana mpango wa kuzifungua leo endapo Ushahidi wa wiki nzima wa kutokuwa na haraka kurejelea shughuli za kawaida ni jambo la kutegemea .

Katika fikra za kila unayezungumza naye,ni kana kwamba ametekwa nyara na kitu kimoja-matokeo ya uchaguzi wa urais.Wengi wanataka mshindi atangazwe ili waendelee na shughuli zao

Katika mji wa Eldoret,eneo la Rift Valley linalochukuliwa kama ngome ya naibu wa William Ruto,mvua ilinyesha usikukucha na wenyeji hawana kasi ya kuamka.

‘Mwendo ni wa pole pole hapa,kwa kawaida watu hurauka alfajiri na mapema kuendelea na shughuli za kawaida lakini leo hali ni tofauti’ Mwandishi wa BBC Robert Kiptoo amesema.

Anaongeza kuwa jana jumapili kulikuwa na shughuli mjini lakini huenda pia zilinoga kwa sababu ilikuwa ni wikendi .

Katika mji wa Kisumu ,magharibi mwa Kenya-ngome ya aliyekuwa Waziri mkuu Raila Odinga ,kuna hamu kubwa ya wenyeji kutaka matokeo kutangazwa.

Pindi tu baada ya uchaguzi siku ya jumanne ,wenyeji wamekuwa wakikusanyika katika vikundi kujadili na kusikiliza kupitia redio kuhusu kinachoendelea .Biashara nyingi pia hazijafunguliwa na wengi watangoja tangazo la IEBC kabla ya hali ya kawaida kurejea katika mji huo .