Makamishna 4 wa IEBC waliopinga matokeo kutoa taarifa

Wanne hao watatoa hotuba yao Jumanne alasiri katika hoteli ya Serena.

Muhtasari

•Wanne hao wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera watatoa hotuba yao Jumanne alasiri katika hoteli ya Serena.

•Jumatatu jioni makamishna hao walijitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais hata kabla ya kutangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati

Makamishna Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya.
Makamishna Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya.
Image: FREDRICK OMONDI

Makamishna wanne wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini ambao walijitenga na matokeo ya urais wanatarajiwa kuhutubia wanahabari.

Wanne hao wakiongozwa na naibu mwenyekiti wa tume Juliana Cherera watatoa hotuba yao Jumanne alasiri katika hoteli ya Serena, jijini Nairobi.

Pamoja na Cherera ni makamishaa; Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyangaya ambao wote waliteuliwa rais Uhuru Kenyatta mwaka jana.

Jumatatu jioni makamishna hao walijitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais hata kabla ya kutangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati

Walifanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli hiyo hiyo ya Serena na kueleza kutoridhishwa kwao na jinsi hatua ya mwisho ya uchaguzi ilivyoendelezwa.

"Tumefanya uchaguzi wa 2022 kwa njia bora zaidi. Tumehakikisha kuwa tumeboresha viwango.  Tumefanya kazi nzuri lakini baadhi ya mambo yanahitaji kuwekwa wazi.Tupo hapa kwa sababu ya hali ya kutoeleweka ambayo hatua ya mwisho ya uchaguzi mkuu huu. Hatuwezi kuchukua umiliki wa matokeo ambayo yanaenda kutangazwa," Cherera alisema.

Naibu mwenyekiti huyo wa IEBC alibainisha kuwa watu ambao hawataridhishwa na matokeo wapo huru kuelekea mahakamani.