Hakuna kura zilizoibiwa! Malala asema huku akikubali kushindwa na kumpongeza Barasa

Pia aliipongeza IEBC kwa kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.

Muhtasari

•"Hakuna kura iliibiwa. Msidanganywe, hakuna kura zilizoibiwa. Matokeo ni halali na ninayakubali," Malala alisema.

•Malala alisema yuko tayari kutoa sehemu yoyote ya manifesto yake ambayo Barasa ataona inafaa katika serikali 

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleopas Malala
Image: MAKTABA

Mgombea Ugavana wa ANC Cleophas Malala amekubali kushindwa katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Kakamega.

Akizungumza siku ya Jumanne, Malala aliwataka wafuasi wake wasidanganywe kuwa kura zake ziliibwa.

"Hakuna kura iliibiwa. msidanganywe, hakuna kura zilizoibiwa. Matokeo ni halali na ninayakubali," Malala alibainisha.

Fernandes Barasa wa ODM alitangazwa mshindi Jumanne katika kinyang'anyiro cha ugavana wa Kakamega baada ya kupata kura 192,768 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Malala aliyepata kura 59,275.

Uchaguzi huo ambao uliahirishwa mara mbili na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ulirekodi idadi ndogo ya wapiga kura.

Barasa alishinda katika maeneo bunge yote ya upande wa kusini na mengine mawili ya upande wa kaskazini, huku Malala akishinda katika maeneo bunge yote ya kati na upande wa kaskazini.

Malala alimpongeza Barasa, akitaja ushindi huo kuwa unastahili na usiopingika.

Alisema yuko tayari kutoa sehemu yoyote ya manifesto yake ambayo Barasa ataona inafaa katika serikali mpya kwa maendeleo ya Kakamega.

Pia aliipongeza IEBC kwa kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.

Akitoa shukrani kwa timu yake ya kampeni, Malala alisema anajivunia kwa kufanikiwa kuwa kwenye debe.

"Tulijitahidi na ninajivunia sana ... sikutarajia kufika hapa," alibainisha.

Seneta huyo wa zamani ana matumaini ya mustakabali mzuri wa kisiasa.

"Njia yetu mbele itaenda mbali na ni hatua ya kutengeneza historia ... nina matumaini kuwa tutafanya vyema zaidi. Tulithubutu kuota,” aliongeza.

Malala pia alitoa shukrani zake kwa wakazi wa Kakamega waliompigia kura.