Mahakama ya Juu kutoa uamuzi kuhusu kura ya Urais leo

Chebukati, alimtangaza Ruto kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 7,176,141 dhidi ya milioni 6,942,930 za Bw Odinga

Muhtasari

• Mgombea aliyeshindwa Raila Odinga anasema kura hiyo ilibadilishwa ili kumpa mpinzani wake William Ruto ushindi mwembamba katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali.

Majaji wa mahakama ya juu
Majaji wa mahakama ya juu

Mahakama ya Juu nchini Kenya leo itatoa uamuzi wake kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.

Majaji saba wa mahakama hiyo walianza kuandaa uamuzi huo siku ya Ijumaa baada ya kuhitimisha kusikilizwa kwa pingamizi iliowasilishwa kwa siku tatu.

Mnamo Agosti 15, siku sita baada ya Uchaguzi Mkuu, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, alimtangaza Dkt Ruto kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 7,176,141 (asilimia 50.49) dhidi ya milioni 6,942,930 za Bw Odinga (asilimia 48.85) )

Prof George Wajackoyah wa Roots Party alifanikiwa kura 61,969 (asilimia 0.44) huku David Mwaure Waihiga wa Agano Party akiibuka wa nne kwa kura 31,987 (asilimia 0.23).

Mgombea aliyeshindwa Raila Odinga anasema kura hiyo ilibadilishwa ili kumpa mpinzani wake William Ruto ushindi mwembamba katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali. Mawakili wa Bw Ruto na tume ya uchaguzi wanakanusha madai hayo.

Hii ni mara ya tatu kwa Bw Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi katika mahakama ya juu. Ruto na Odinga wamesema wataheshimu uamuzi wa mahakama kuhusu ombi la urais. Majaji wataegemeza uamuzi wao juu ya masuala tisa ambayo yaliangaziwa katika ombi lililowasilishwa.

Wachambuzi wanasema tofauti na mamlaka nyingine, ni vigumu kutabiri jinsi majaji watakavyotoa amri yao kwa kuzingatia historia, itikadi au falsafa zao. Wataalamu wa sheria wametaja hali tatu zinazowezekana kuegemea uamuzi huo.

Wanasema kuwa majaji hao saba wanaweza kuidhinisha uchaguzi wa rais mteule William Ruto, kubatilisha uchaguzi huo, na kuagiza ushindi wa marudio au kukabidhiwa kwa mlalamishi, Bw Odinga.

Uamuzi wa Jumatatu unaweza kubadilisha hali ya kisiasa ya nchi na pia kutoa fursa ya kurekebisha sheria za uchaguzi za nchi.

Wagombea wote wawili wameahidi kuheshimu uamuzi wa mahakama kuu.

William Ruto
William Ruto

Dkt Ruto alisisitiza heshima kwa taasisi huru. Aliwaambia viongozi wa kisiasa kuziruhusu taasisi hizo kutekeleza majukumu yao "bila vitisho, shuruti na usaliti".

"Ili kusisitiza kuhusu demokrasia yetu, kipaumbele chetu kama utawala ni kuwa na mahakama inayofanya kazi vyema, yenye ufanisi na huru itakayolinda maslahi ya umma na kulinda Katiba yetu," Dkt Ruto aliuambia ujumbe wa Majaji na Wanasheria wa Afrika uliumtembelea nyumbani kwake huko Karen.

Bw Odinga, kwa upande mwingine, anaamini kuwa uchaguzi wa urais wa Agosti 9 ulikumbwa na dosari nyingi, akiongeza kwamba alichokuwa akitafuta ni "ukweli" tu na kwamba angerejea nyumbani ikiwa angepoteza uchaguzi huo kwa haki.

"Tunaomba mahakama itoe haki na nina hakika kwamba sikushindwa na kwa hivyo nitasimama kidete na sitatikiswa hadi sauti ya watu wa Kenya kama ilivyotolewa Agosti 9 iheshimiwe," Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) aliambia waumini katika Kanisa la Kibra African Inland Jumapili iliyopita.

Raila Odinga
Raila Odinga

Wakati huo huo, usalama umeimarishwa katika eneo la mahakama huku sehemu za barabara zikifungwa kabla ya hukumu hiyo. Naibu afisa mkuu wa polisi nchini Kenya amewashauri wananchi kufuata matangazo ya majaji hao katika runinga majumbani mwao.