Ruto vs Raila: Mwelekeo upi utafuatwa baada ya mahakama kufuta au kudhinisha uchaguzi wa urais

Mahakama ya upeo inaweza kuidhinisha ama kubatilisha matokeo ya urais.

Muhtasari

•Iwapo mahakama itaamua kuwa matokeo yaliyotangazwa mnamo Agosti 15 ni ya halali na kushikilia ushindi wa Ruto, hiyo ina maana kwamba naibu rais huyo  anayeondoka atakuwa tayari kuapishwa.

•Iwapo mahakama itaamua kutupilia mbali matokeo hayo, basi hakutakuwa na budi ila kurudi debeni kwa mara nyingine kumchagua rais mpya. 

Jaji Mkuu Martha Koome
Image: BBC

Leo hii, Jumatatu Septemba 9 Mahakama ya Upeo inatarajiwa kutoa maamuzi yake kuhusu kesi ya urais iliyosikilizwa wiki jana.

Wiki iliyopita majaji saba wa Mahakama ya Upeo; CJ Martha Koome, DCJ Philomena Mwilu, Njoki Ndung'u, Smokin Wanjala, Isaac Lenaola na William Ouko waliwasikiliza mawakili kutoka upande wa  Raila Odinga, William Ruto na IEBC na wahusika wengine kisha baadae kuchukua mapumziko ili kuandika hukumu watakayotoa.

Majaji hao walitumia wikendi nzima kuandika uamuzi wao kuhusu masuala tisa yaliyowasilishwa mahakamani siku tatu zilizopita katika ombi la kupinga kuchaguliwa kwa Naibu Rais William Ruto kuwa Rais Mteule.

Mnamo Agosti 15, siku sita baada ya Uchaguzi Mkuu, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa Rais mteule baada ya kuzoa kura 7,176,141 (50.49%) dhidi ya milioni 6,942,930 za Raila (48.85%).

Baadae Raila alielekea katika mahakama ya upeo na kupitia mawakili wake akadai kuwa kura hiyo ilibadilishwa ili kumpa ushindi mwembamba mpinzani wake William Ruto katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali. Mawakili wa Bw Ruto na tume ya uchaguzi hata hivyo wamekanusha madai hayo.

Kesi hiyo ilianza Jumanne kwa kongamano la kabla ya kesi baada ya walalamishi na walalamikiwa kumaliza kuwasilisha hati zao za kiapo kufikia Jumatatu. 

Baada ya kusikiliza pande zote zinazohusika katika kesi hiyo, mahakama ya upeo inatarajiwa kutoa uamuzi wa iwapo ushindi wa Ruto katika kinyang'anyoro cha Agosti 9 ulikuwa halali au kulikuwa na udanganyifu.

Katika uamuzi ambao umepangwa kutolewa kuanzia saa sita mchana, Mahakama ya Upeo inaweza kuamua:-

i) Kuidhinisha matokeo ya urais.

ii) Kubatilisha matokeo ya urais.

Iwapo mahakama itaamua kuwa matokeo yaliyotangazwa mnamo Agosti 15 ni ya halali na kushikilia ushindi wa Ruto, hiyo ina maana kwamba naibu rais huyo  anayeondoka atakuwa tayari kuapishwa.

Kuapishwa kwa rais mteule kunafaa kufanyika siku saba baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wake. Hii ni kumaanisha kuwa iwapo mahakama itaidhinisha ushindi wa Ruto basi ataapishwa tarehe 15 Septemba. 

Kwa upande mwingine, iwapo mahakama itaamua kutupilia mbali matokeo hayo, basi hakutakuwa na budi ila kurudi debeni kwa mara nyingine kumchagua rais mpya. 

Kisheria, matokeo ya urais yanapobatilishwa, uchaguzi mwingine unapaswa kuandaliwa ndani ya siku 60 baada ya uamuzi kutolewa. Hii ni kumaanisha tume ya uchaguzi inapaswa kuandaa uchaguzi mwingine wa urais kabla ya Novemba 4, 2022.

Mwaka wa 2017 mahakama hiyo iliweka historia kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kubatilisha uchaguzi wa rais.