(+Picha) Rais Uhuru amtembelea Raila baada ya Mahakama kuidhinisha ushindi wa Ruto

Uhuru alishiriki mkutano na kinara huyo wa ODM Jumanne jioni.

Muhtasari

•Uhuru alishiriki mkutano na kinara huyo wa ODM Jumanne jioni ambapo walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali ambayo hayakufichuliwa.

•Haya yalijiri siku moja tu baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Ruto katika kinyang'anyiro cha urais cha Agosti 9.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Rais Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu katika Wizara ya Masuala ya ndani Karanja Kibicho
Image: HISANI

Siku ya Jumanne Rais Uhuru Kenyatta alimtembelea mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Odinga katika makazi yake rasmi ya Karen, Nairobi.

Uhuru alishiriki mkutano na kinara huyo wa ODM Jumanne jioni ambapo walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali ambayo hayakufichuliwa.

Rais alikuwa ameandamana na mwanawe Muhoho Kenyatta katika ziara hiyo. Familia ya Raila akiwemo mkewe Ida Odinga, binti yake Winnie Odinga na kakake mkubwa Oburu Odinga pia walikuwepo.

Viongozi wengine ambapo walikuwepo kwenye kikao ni pamoja na nduguye Raila Oburu Odinga, gavana wa Siaya James Orengo, Katibu Mkuu katika Wizara ya Masuala ya ndani Karanja Kibicho, msemaji wa sekretarieti ya urais ya Raila Makau Mutua, wakili Paul Mwangi miongoni mwa wengine.

Haya yalijiri siku moja tu baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Ruto katika kinyang'anyiro cha urais cha Agosti 9.

Siku ya Jumatatu, jopo la majaji saba wa Mahakama ya Upeo kwa kauli moja lilitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya urais yaliyopendelea mgombea wa Kenya Kwanza William Ruto na kusema kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha.

Katika hukumu iliyosomwa na Jaji Mkuu Martha Koome, mahakama iliyaidhinisha matokeo ya urais ambayo yalitangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mnamo Agosti 15.

“Huu ni uamuzi wa pamoja. Malalamishi hayo yametupiliwa mbali, kwa hivyo tunamtangaza mlalamikiwa wa kwanza (Ruto) kuwa rais mteule,” Koome alisema.

Kuidhinishwa kwa ushindi wa Ruto kulimaanisha kuwa Raila sasa amepoteza katika majaribio yake yote matano ya kuwania urais.

Hii imewaacha mamilioni ya wafuasi wake katika hali ya sintofahamu kuhusu hatua inayofuata ikizingatiwa kuwa  huenda hilo lilikuwa jaribio lake la mwisho la kutwaa kiti hicho cha juu zaidi nchini. 

Hapo awali kiongozi huyo wa ODM aliwahi kusema kuwa hatawania urais tena iwapo angepoteza uchaguzi wa mwaka huu.