- Murkomen na Seneta wa Nandi Samson Cherargei walitoa salamu zao za pongezi mapema kwa Kisang
Chama cha UDA bado kimeibuka na ushindi kwani mgombeaji wake William Kisang alishinda kiti cha Useneta wa Elgeyo Marakwet.
Kisang alipata kura 41,378 katika uchaguzi mdogo wa Alhamisi, Tim Kipchumba wa chama cha PPD aliibuka wa pili kwa kura 38,151.
Kiti hicho kilivutia wagombea wengine wanne; Jerotich Seii wa chama cha Safina, wagombeaji huru Andrew Mengich na Kelvin Kemboi na Timothy Tanui wa New Democrats Party.
Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya aliyekuwa Seneta Kipchumba Murkomen kuteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi na Rais William Ruto mnamo Oktoba 2022.
Wagombea wawili, Tim na Seii, walikuwa tayari wamekubali kushindwa kabla ya matokeo kutangazwa na IEBC.
Murkomen na Seneta wa Nandi Samson Cherargei walitoa salamu zao za pongezi mapema kwa Kisang.
"Hongera William Kisang kwa kuchaguliwa kwako kama seneta wa pili wa Elgeyo Marakwet. Asante wakazi wa Elgeyo Marakwet kwa kumheshimu Dkt William Ruto na udugu wa Kenya Kwanza," Cherargei alisema.
"Hongera William Kisang kwa kuchaguliwa kwako kama seneta wa pili wa Elgeyo Marakwet. Asante kwa watu wa Elgeyo Marakwet kwa kuwa na imani na uongozi wa Kenya Kwanza kwa kumpigia kura mgombeaji wa UDA," Murkomen alisema.