Fahamu jinsi unavyoweza kushiriki kwenye mdahalo wa manaibu rais

Mdahalo huo utafanyika Julai 19 kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa nne jioni.

Muhtasari

•Mdahalo wa Manaibu Rais ambao utafanyika Julai 19 katika chuo cha CUEA uko wazi kwa wananchi.

•Wapiga kura wanaotaka kushiriki wanaombwa kuwasilisha maswali yao kupitia ujumbe mfupi kwenye nambari 22843.

Martha Karua na Rigathi Gachagua
Image: MAUREEN KINYAJUI

Mdahalo wa Manaibu Rais, utakaofanyika Julai 19 uko wazi kwa wananchi, waandalizi wametangaza.

Mdahalo huo utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) utafanyika kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa nne jioni.

Wagombea wenza wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Agosti 9 ni pamoja na Rigathi Gachagua wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua,Martha Karua wa Azimio la Umoja-One, Justina Wamae wa Roots Party na Ruth Mucheru Mutua wa chama cha Agano

Wapiga kura wanaotaka kushiriki wanaombwa kuwasilisha maswali yao kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye nambari 22843.

Pia, maswali yanaweza kutumwa kama  video kwa Nambari ya WhatsApp 0796560560 lakini video inapaswa kuwa chini ya sekunde 30.

Katika taarifa iliyotolewa wiki hii, kikao kitakachowakutanisha Gachagua na Karua kitasimamiwa na Sophia Wanuna wa KTN News na James Smart wa NTV.

Kikao hicho kitafanyika kati ya saa mbili na saa tatu unusu usiku wa Jumanne.

Hata hivyo, Ijumaa mkurugenzi wa mawasiliano ya kampeni ya Urais katika kambi ya Kenya Kwanza Hussein Mohammed alieleza kuwa Gachagua ndiye atakayeamua kama atahudhuria mdahalo huo au la.

"Iwapo mgombeaji (Ruto) na mgombea mwenza watajitokeza au la ni suala ambalo liko kwao kabisa," alisema.

Mdahalo wa wawili hao utatanguliwa na mdahalo kati ya wagombea wenza wa wagombea urais ambao walipata chini ya asilimia 5 katika kura tatu za maoni za hivi majuzi.

Kikao kinachowakutanisha Justina Wamae wa chama cha Roots na Ruth Mutua wa Agano kitasimamiwa na mtangazaji wa TV47 Linda Alela na Jacob Kioria wa KBC.

Trevor Ombija wa runinga ya Citizen atasimamia mijadala itakayofanyika kabla na baada ya midahalo yote miwili.

Wasimamizi watahitajika kutekeleza majukumu fulani na kuzingatia sheria fulani.

(Utafsiri: Samuel Maina)