Fahamu stakabadhi ambazo Ruto amewasilisha kwa IEBC leo

Muhtasari

• Ruto alifika katika eneo la Bomas of Kenya jijini Nairobi Jumamosi asubuhi kuwasilisha karatasi zake mbele ya IEBC ili kupata kibali cha kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

•Baada ya kuwasilisha karatasi zake, Ruto ataingia jijini kuzuru mitaa mbalimbali jijini Nairobi

Naibu rais William Ruto akiongoza mkutano wa IBEC, Jumanne.
Naibu rais William Ruto akiongoza mkutano wa IBEC, Jumanne.
Image: twitter.com/WilliamsRuto

Naibu Rais William Ruto alifika katika eneo la Bomas of Kenya jijini Nairobi Jumamosi asubuhi kuwasilisha karatasi zake mbele ya wakuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili kupata kibali cha kuwania urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua walisindikizwa na viongozi kadhaa wa Kenya Kwanza na mamia ya wafuasi wao.

Alifika mwendo wa saa nne alfajiri na anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zifuatazo kwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati saa tano asubuhi;

  • Nakala zilizothibitishwa za vyeti vya elimu

 

  • Nakala iliyoidhinishwa ya kitambulisho au pasipoti

 

  • Picha saizi ya pasipoti, karatasi na nakala ya kompyuta.

 

  • Barua ya kuachakazi kutoka kwa mwajiri wa zamani

 

  • Cheti cha uteuzi kutoka kwa chama kilichosajiliwa

 

  • Kanuni za maadili zilizotiwa saini ipasavyo

 

  • Sahihi 2,000 kutoka angalau kaunti 24

 

  • Ada ya uteuzi Sh200,000.

Baada ya kuwasilisha karatasi zake, Ruto ataingia jijini kuzuru mitaa mbalimbali jijini Nairobi kisha amalizie katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji lililo eneo bunge la Kamukunji.

Atakuwa akijipigia debe na vilevile kuwafanyia kampeni wagombeaji wake wa Kenya Kwanza wakati wa ziara yake.

Msafara wa Ruto utasimama angalau katika vituo saba ambapo atauza mtindo wake wa kiuchumi wa chini kwenda juu.

Ataanzia South C, South B, Mukuru, City Stadium, Gikomba, Majengo na hatimaye Kamukunji.

Ruto aliingia katika siasa wakati akimfanyia kampeni mgombeaji urais wa Kanu Daniel arap Moi chini ya vuguvugu la Youth for Kanu '92.

Miaka mitano baadaye, aliwania kiti cha ubunge cha Eldoret Kaskazini mnamo 1997 baada ya yeye na vijana wengine mahiri kuwa 'waasi' wa Kanu na akashinda.

Mnamo 2002, Ruto alifanikiwa kutetea kiti chake. Mwaka wa 2006, Ruto alitangaza kuwa atawania urais.

Hili halikuwaendea vyema  wanasiasa wa Kanu, akiwemo Rais wa zamani Moi, ambaye alilaani uamuzi wake mara moja.

Akiwa amekasirishwa, Ruto alivuka hadi ODM ambako alijaribu kupata tikiti ya chama kuwania urais.

Akiwa mshirika mkubwa wa Raila katika uchaguzi wa 2007, Ruto alionyesha msukosuko wake wa kisiasa alipoongoza wimbi la ODM lililokumba Rift Valley kutwaa viti vyote.