Huna mamlaka ya kumfundisha Ruto!- Gachagua akabiliana na Karua

Muhtasari

•Hii ni baada ya Karua kumkashifu Ruto kuhusu ripoti iliyoashiria kuwa atamchunguza Rais Uhuru Kenyatta iwapo atashinda urais.

•Gachagua alisema Karua hajawahi kumheshimu rais Uhuru wala kumuunga mkono na kwa hivyo hapaswi kuwafundisha chochote kuhusiana naye

Naibu Rais William Ruto akiwa na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua wakati wa mkutano wa hadhara huko Githunguri, Kiambu Ijumaa, Februari 18, 2022.
Naibu Rais William Ruto akiwa na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua wakati wa mkutano wa hadhara huko Githunguri, Kiambu Ijumaa, Februari 18, 2022.
Image: Picha: DPPS

Mgombea mwenza wa muungano wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua amemjibu mwenzake wa Azimio la Umoja-One Kenya Martha Karua kufuatia shambulio dhidi ya bosi wake William Ruto.

Hii ni baada ya Karua kumkashifu Ruto kuhusu ripoti iliyoashiria kuwa atamchunguza Rais Uhuru Kenyatta iwapo atashinda kiti cha urais kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Shambulio hilo dhidi ya Naibu Rais linaonekana  kumkasirisha Gachagua ambaye alimtupia vijembe Karua akimwambia aepuke vita vinavyomgombanisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake.

Gachagua alisema Karua hajawahi kumheshimu rais Uhuru wala kumuunga mkono na kwa hivyo hapaswi kuwafundisha chochote kuhusiana naye.

"Dada yangu huna uwezo wala mamlaka ya kimaadili ya kumfundisha William Ruto kuhusu kumheshimu Uhuru Kenyatta. Usingejua jinsi ya kumheshimu Uhuru Kenyatta kwa sababu hujawahi kumheshimu au kumuunga mkono," Gachagua alisema.

"Unahitaji mafunzo ukuje mimi nikukalishe chini nikufundishe njia ya kuunga mkono na kupatia yeye heshima kwa sababu tunaelewa."

Alikuwa akihutubia ibada katika kanisa la St Thomas The Apostle huko Meru siku ya Jumapili.

Akitoa hotuba katika kaunti ya Nyandarua siku ya Jumamosi, Karua alitaja Ruto kama mtu ambaye hafai kwa uongozi.

Alitaja mpango wa DP kumchunguza Uhuru iwapo atashinda urais kama ishara tosha kwamba hataongoza Wakenya vyema.

"Kiongozi yeyote anayetishia mtu binafsi awe rais au mtu mwingine yeyote hafai kuchaguliwa kuwa kiongozi," Karua alisema.

Gachagua pia alimkumbusha Karua kwamba eneo la Mlima Kenya liko nyuma ya DP.

Alimkemea akisema ana tabia ya kuchukua mwelekeo tofauti kisiasa wakati eneo hilo lina msimamo mmoja kuhusu ni nani watampigia kura.

"Amerudia anachofanya kila baada ya miaka mitano. Yeye hutembea kila mara kinyume na mahali ambapo watu wa Mlima Kenya wanatembea," alisema.

DP na timu yake watapiga hema katika Kaunti ya Meru Jumapili hii ili kuunga mkono azma yao ya urais.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki miongoni mwa viongozi wengine.