Jimi Wanjigi anyimwa kibali cha kuwania urais wa Kenya

Muhtasari

•Chebukati amesema mgombea urais huyo alikosa kutimiza idadi ya saini za wafuasi zilizohitajika ili kupatiwa kibali. 

•Mfanyibiashara huyo amewahakikishia wafuasi wake kuwa ataelekea mahakamani katika juhudi za kupinga uamuzi huo.

Jimi Wanjigi
Jimi Wanjigi
Image: EUTYCAS MUCHIRI

Mgombea urais kwa tikiti ya Safina Jimi Wanjigi amekosa kuidhinishwa kushiriki katika kinyang'anyiro cha mwezi Agosti.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema mgombea urais huyo alikosa kutimiza idadi ya saini za wafuasi zilizohitajika ili kupatiwa kibali. Pia alisema kulikuwa na shida na vitambulisho alivyowasilisha.

Chebukati pia alisema mgombea urais huyo alikosa kuwasilisha cheti chake cha shahada ya chuo kikuu.

"Tumewaruhusu wengine wenye matatizo na sahihi kufanya marekebisho, na pia tunaweza kukuruhusu kufanya hivyo katika saa zilizobaki.. Lakini lazima ulete nakala halisi ya cheti chako cha shahada kabla sijakuondoa," Chebukati alimwambia Wanjigi.

Pia alisema Wanjigi aliambatanisha nakala zake za elimu kinyume na kanuni zinazosema kwamba kila mgombeaji lazima awasilishe cheti kutoka kwa taasisi inayotambulika nchini.

Wanjigi ambaye alikuwa amendamana na mgombea mwenza wake Willis Otieno pia alitupilia mbali uamuzi wa IEBC huku akidai kuwa kuna njama ya kisiasa inayolenga kumzuia kuwania urais.

"Ni wazi kinachoendelea hapa. Kuna mchujo wazi kabisa ambao unaamuliwa kwingine si hapa," Wanjigi alisema.

Alidai kuwa baadhi ya wagombea urais waliidhinishwa na tume bila maswali baada ya kuwasilisha stakabadhi zao katika muundo sawa na yeye.

Chebukati hata hivyo alimwelekeza Wanjigi kutumia mchakato wa kusuluhisha mzozo ikiwa anahisi kutoridhika.

"Huu ni uamuzi wangu na ikiwa una masuala yoyote tuna kamati ya kutatua mizozo," Chebukati alisema.

Wanjigi amewahakikishia wafuasi wake kuwa ataelekea mahakamani katika juhudi za kupinga uamuzi huo.

"Ningependa kuwahakikishia wafuasi wetu kuwa nitakuwa debeni katika uchaguzi wa Agosti 9. Hawataepuka," Wanjigi alisema.