Kakake Moses Kuria aibua madai ya wizi wa kura katika kinyang'anyiro cha ubunge Juja

Kinyajui anasema kuwa zoezi zima lilikuwa la uzushi.

Muhtasari

•Kinyanjui ambaye kwa sasa yupo nyuma ya mbunge wa sasa George Koimburi wa UDA anasema kuwa zoezi zima lilikuwa la uzushi.

•Moses Kuria ambaye alikuwa akiwania ugavana wa  Kiambu kwa tikiti ya Chama Cha Kazi tayari amekubali kushindwa.

Image: FACEBOOK// ALOISE KINYAJUI

Kakake Moses Kuria, Aloise Kinyanjui, ambaye anawania kiti cha ubunge Juja kwa tikiti ya Jubilee ametishia kuelekea mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika eneo hilo.

Kinyanjui ambaye kwa sasa yupo nyuma ya mbunge wa sasa George Koimburi wa UDA anasema kuwa zoezi zima lilikuwa la uzushi.

Kinyanjui kupitia ujumbe wa Facebook amesema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC itakuwa mlalamikiwa wa kwanza katika kesi yake.

Iwapo Koimburi atashinda kiti hicho itakuwa ni mara ya pili kwa chama cha Jubilee kupoteza kiti hicho kwa UDA katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Koimburi alimwabwaga chini mke wa aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, marehemu Francis Munyua, Susan Njeri ambaye alikuwa akiwania kwa tikiti ya Jubilee wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika Mei 18, 2021.

Kakake Kinyanjui, Moses Kuria ambaye alikuwa akiwania kiti cha Ugavana wa Kiambu kwa tikiti ya Chama Cha Kazi tayari amekubali kushindwa.