Magavana wateule Barasa, Nassir kuapishwa Septemba 15

Magavana waliochaguliwa wanastahili kuapishwa siku 10 baada ya kutangazwa washindi.

Muhtasari

•Hii ni baada ya kaunti hizo mbili kuwachagua wakuu wao wapya mnamo Agosti 29, 2022, baada ya uchaguzi kuahirishwa mara mbili.

•Kuapishwa kunapaswa kufanyika siku ya Alhamisi ya kwanza baada ya kupita siku kumi.

Mgombea wa ODM Abduswamad Nassir na mgombea mwenza Francis Thoya washerehekea baada ya kupewa cheti cha IEBC na msimamizi wa uchaguzi kaunti ya Mombasa Swalha Yusuf siku ya Jumanne.
Mgombea wa ODM Abduswamad Nassir na mgombea mwenza Francis Thoya washerehekea baada ya kupewa cheti cha IEBC na msimamizi wa uchaguzi kaunti ya Mombasa Swalha Yusuf siku ya Jumanne.
Image: JOHN CHESOLI

Magavana wateule wa Kakamega na Mombasa wataapishwa mnamo Septemba 15, 2022, kwa mujibu wa sheria.

Hii ni baada ya kaunti hizo mbili kuwachagua wakuu wao wapya mnamo Agosti 29, 2022, baada ya uchaguzi kuahirishwa mara mbili.

 Katika kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Nassir wa ODM alishinda kinyang'anyiro cha ugavana huku Fernandes Barasa akishinda Kakamega.

Kwa mujibu wa sheria, magavana wote wapya waliochaguliwa wanastahili kuapishwa siku 10 baada ya kutangazwa washindi na IEBC.

Kuapishwa kunapaswa kufanyika siku ya Alhamisi ya kwanza baada ya kupita siku kumi.

"Gavana Mteule, wakati wa hafla ya kuapishwa, atakula kiapo au uthibitisho wa afisi kama ilivyoainishwa katika sehemu ya Ratiba ya Kwanza ya Sheria ya Kuchukua Ofisi ya Gavana 2019," inasema sheria hiyo.

Magavana 45 waliapishwa mnamo Agosti 25, 2022.

Sheria inaeleza kwamba kiapo au uthibitisho utafanyika si kabla ya saa nne asubuhi na si baada ya saa nane alasiri.

"Gavana Mteule, wakati wa hafla ya kuapishwa, atakula kiapo au uthibitisho wa ofisi kama ilivyoainishwa katika Ratiba ya Kwanza ya Sheria ya Kuchukua Ofisi ya Gavana 2019," inasema sheria hiyo.

Hata hivyo, zoezi hilo litafanyika mara baada ya washindi wa viti vya kaunti kutangazwa kwenye gazeti la serikali na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Jaji Mkuu Martha Koome alikuwa tayari amewateua majaji 47 ambao watasimamia uapisho huo.

Sheria inasema kuwa kuapishwa kwa gavana mteule kutafanyika katika hafla ya hadhara mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu.

Huko Mombasa, Jaji George Dulu ataongoza hafla hiyo huku Kakamega akiwa Jaji Dora Chepkwony.