Pastor Ng'anga amkejeli Mwaure kwa kushindwa na "mtu wa bangi"

Ng'ang'a amemtaka Mwaure kugura siasa na kurejelea kazi ya kuhubiri neno la Mungu kwa wakristo.

Muhtasari

•Ng'ang'a amemtaka mgombea urais huyo kugura siasa na kurejelea kazi ya kuhubiri neno la Mungu kwa wakristo.

•"Naona kuna Bishop yuko hapo na huyu wa ma***de ndiye ako na kura nyingi. Ngai! na ni Bishop! Ulienda kubaya. Huko ni nje Askofu, rudi kwa kanisa," Ng'ang'a alisema.

Pastor James Ng'ang'a na mgombea urais David Mwaure
Image: MAKTABA

Mchungaji maarufu James Ng'ang'a wa Neno Evangelism Center amemkejeli mgombea urais wa chama cha Agano David Mwaure kwa kushindwa kura na Profesa George Wajackoyah wa Roots Party.

Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa lake, Ng'ang'a amemtaka mgombea urais huyo kugura siasa na kurejelea kazi yake ya awali ya kuhubiri neno la Mungu kwa wakristo.

"Naona kuna Bishop yuko hapo na huyu wa ma***de ndiye ako na kura nyingi. Ngai! na ni Bishop! Ulienda kubaya. Huko ni nje Askofu, rudi kwa kanisa," Ng'ang'a alisema.

Kasisi huyo mwenye utata alidokeza kuwa Wajackoyah amepata kura kadhaa kutoka sehemu mbalimbali za nchi tofauti na Mwaure ambaye hakupata kura nyingi.

"Amekaa miaka 40. Baada ya miaka 40 askofu ametokezea leo na huyu wa bangi pia akatokezea. Bishop amenyoa, amevaa suti alafu huyu amevaa tu kakofia!" Alisema Ng'ang'a.

Kulingana na matokeo rasmi ya IEBC yaliyotolewa kama ilivyo sasa, Waihiga anavuta mkia miongoni mwa wagombea wagombea wote wa urais akiwa amepata kura 28,700 pekee kutoka maeneo bunge 253.  Wajackoyah ameshikilia nafasi ya tatu kwa kura 56,000.

Hili ni jaribio la kwanza la Mwaure kuwania kiti cha urais wa Kenya. Kitaaluma yeye ni wakili na mtumishi wa Mungu.

Jumapili, mgombea urais huyo wa Agano Party alijitokeza kukubali matokeo kushindwa baada ya kile alichotaja kuwa "kuona matokeo hayaegemei upande wao, wameamua kukubali kwamba hiki kiti si chao."

Akizungumza na wanahabari, Mwaure alisema kwamba baada ya kuona matokeo jinsi yanavyozidi kutolewa na IEBC na kujadiliana kwa undani na wanachama, wameamua kukubali mapema hata kabla ya mchakato mzima wa kuhesabu kura haujakamilika rasmi katika ukumbi wa Bomas.

“Tunachukua hatua hii baada ya kuona jinsi tulivyofanya katika uchaguzi na pia baada ya kujadili na timu yetu pale Bomas. Pia tumekuwa tukifuatilia jinsi mchakato wa kuhesabu wa kudhibitisha kura umekuwa ukiendelea kwenye ukumbi wa Bomas na kwamba takwimu zile zimekuwa zikimuegemea William Ruto, ambaye ni naibu wa sasa wa Kenya. Sasa hivi tukikubali matokeo, kitu ambacho tumefanya, tungependa kuwashukuru familia zetu, na timu ya kampeni zetu kwa kusimama na sisi,” Mwaure alisema.

Mhubiri huyo vile vile alizidi mbele kuisihi tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kusimama imara na kutopindishwa na vikwazo au vitisho vyovyote kutoka kwa mrengo wowote kwani Wakenya wanatarajia matokeo ya ukweli na haki.

“Tukiwa tumejitoa katika mbio hizo, tungependa kumpendekeza yule anayeonekana kuwa kifua mbele, Dkt William Samoei Ruto na kuitaka IEBC kusimama imara kumtangaza kuwa mshindi wakati wake ukifika, mimi na mgombea mwenza wangu sasa tumetangaza kwamba tutaungana naye William Ruto na kumuunga mkono sio tu kwa sababu anashinda ila pia manifesto yake inawiana na yenu,” Mwaure alisema.