•Chebukati katika taarifa yake alisema tume ya uchaguzi na mipaka itamtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais Jumatatu saa tisa alasiri.
Naibu Rais William Ruto na mkewe Rachael Ruto wameondoka nyumbani kwao Karen kuelekea Bomas of Kenya kabla ya matokeo ya urais kutangazwa na IEBC.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika barua kwa vyombo vya habari alisema tume ya uchaguzi na mipaka itamtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais Jumatatu saa tisa alasiri.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inakualika kuangazia tangazo la Matokeo ya Urais mnamo Jumatatu Agosti 15, 2022 katika Bomas of Kenta saa tisa alasiri," Barua iliyoachiwa na IEBC ilisoma.
Chebukati anatarajiwa kumtangaza rais mpya wa Kenya baada ya shughuli ya uhakiki wa fomu za matokeo ya urais kutoka maeneobunge yote na ujumuishaji wa kura kukamilika.
Uhakiki wa fomu za matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9 ulikamilika Jumatatu asubuhi baada ya kuendelezwa kwa siku tano.
Hapo awali, kiongozi wa Roots Party George Wajackoyah na David Mwaure wa Agano walifika katika ukumbi wa Bomas of Kenya kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo.
Kwa sasa, kwaya ya kikatoliki inawaburudisha wanasiasa na waalikwa wengine katika kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura.
Siku ya Jumapili, wagombeaji wawili wakuu wa urais- Raila Odinga na Ruto- walihudhuria ibada tofauti za kanisa huko Karen na kuwataka wafuasi wao kudumisha utulivu na uvumilivu hata wasiwasi kuhusu kura ukizidi kupamba moto.