Wajackoyah agura ukumbi wa mdahalo wa urais baada ya madai yake kutotimizwa

Wajackoyah alitaka wagombea wote wanne wa urais kuwa na mdahalo wa pamoja

Muhtasari

•Wajackoyah alikuwa amefika katika ukumbi huo kuteta kuwa sekretarieti ya mdahalo wa urais haikuwa ikijibu barua zake.

•Aliambia wanahabari kuwa hakuwepo kushiriki katika mjadala huo lakini kuthibitisha kama madai yake yametimizwa au la.

Mgombea urais wa Chama cha Roots George Wajackoyah katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki mnamo Julai 26, 2022.
Mgombea urais wa Chama cha Roots George Wajackoyah katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki mnamo Julai 26, 2022.
Image: PRESIDENTIAL DEBATE SECRETARIAT

Mgombea urais wa Roots Party George Wajackoyah ameondoka katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki ambako mdahalo wa urais umepangwa kuanza.

Wajackoyah alikuwa amefika katika ukumbi huo kutafuta hadhira huku akiteta kuwa sekretarieti ya mdahalo wa urais haikuwa ikijibu barua zake kuhusu jinsi mjadala huo utakavyofanyika.

Alitaka wagombea wote wanne wa urais kuwa na mdahalo wa pamoja kinyume na mijadala ya awamu mbili iliyopangwa na sekretarieti.

"Nimeenda kwa ofisi," Wajackoyah alisema baada ya kusimama kidogo katika njia ya kutoka nje ya ukumbi huo.

Alikuwa amesimama ili kununua picha yake kutoka kwa mchoraji aliyekuwa amesimam kando ya barabara.

Awali bosi huyo wa chama cha Roots alifika katika eneo la mdahalo akiandamana na mgombea mwenza Justina Wamae.

Aliambia Vyombo vya Habari kuwa hakuwepo kushiriki katika mjadala huo lakini kuthibitisha kama madai yake yametimizwa au la.

"Sitajadili isipokuwa tukiwa wanne, hilo ndilo nimekuja kuthibitisha, hawakuwahi kujibu barua yangu," Wajackoyah alisema.

"Kama vyombo vya habari vinataka kuharibu akili ya jamii hii, kama vyombo vya habari vinataka kuendesha ufisadi katika nchi hii, kama vyombo vya habari vyenyewe vinaweza kufanya walichofanya, wakwende huko," alisema.

(Utafsiri: Samuel Maina)