Patanisho: Jamaa akataa kurudi nyumbani baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando

Abigael alisema mumewe alianza kukosekana nyumbani baada ya kuanza mahusiano na mfanyikazi mwenzake

Muhtasari

•Abigael alisema ndoa yao ilivunjika takriban miezi miwili iliyopita baada ya kugundua kuwa mumewe ana mpenzi mwingine.

•Baada ya mumewe kukiri kuwa mwanamke huyo ni kila kitu kwake, Abigael alifanya maamuzi ya kurudi kwao.

•Mike alidai  kuwa alianza kujitenga na mkewe na kutorudi nyumbani baada ya kugundua mabadiliko kadhaa kwake.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Abigael alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Mike Mbuvi.

Abigael alisema kitumbua kiliingia mchanga takriban miezi miwili iliyopita baada ya kugundua kuwa mumewe ana mpenzi mwingine.

Alidai kuwa mumewe alianza kujitenga naye na kukosekana nyumbani mapema mwaka huu wakati alipojitosa kwenye mahusiano na mfanyikazi mwenzake.

"Alianza tabia hii mapema mwaka huu. Alikuwa anaendakazini alafu anamaliza siku mbili tatu bila kurudi nyumbani. Nilimuuliza kwani ni kazi gani hiyo ambayo ilifanya asirudi nyumbani. Alisema kuna kazi  nyingi ambayo alikuwa anafanya," Abigael alisimulia.

"Mwezi wa tano niliona amekithiri nikaenda kazini kwao. Kufika nilimpata na mwanamke ambaye huwa wanatembea kila mahali na hata kuenda kula chakula pamoja. Aliniambia mwanamke huyo ni kila kitu kwake,"

Baada ya mumewe kukiri kuwa mwanamke huyo ni kila kitu kwake, Abigael alifanya maamuzi ya kurudi kwao ila wazazi wa Mike wakamshauri asiende.

"Tuko na ploti Bungoma. Nilihamia kwa hizo ploti zetu. Nilimwambia kuwa sipo nyumbani. Hajawahi kunitembelea," Alisema.

Abigael pia alidai kwamba mumewe tayari amedokeza mpango wa kuoa mke wa pili.

Mike alipopigiwa simu alijitetea kwa kudai kuwa hali ya kazi yake inamzuia kufika nyumbani mara kwa mara.

"Mimi huwa nafanya kazi ya ofisi huko Bungoma. Wakati mwingine inafika kazi inakuwa mingi," Alisema.

Mike alidai  kuwa alianza kujitenga na mkewe na kutorudi nyumbani baada ya kugundua mabadiliko kadhaa kwake.

"Ilifika mahali nikaona hueleweki. Nilianza kuona ni kama unanicheza kidogo," Alisema Mike.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa yupo tayari kushiriki kikao na Abigael katika juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo wao.

"Niko tayari tuongee tuone vile tutasuluhisha maneno hayo... Nitakuwa nashika simu zako tukiongea tuelewane," Alisema

Wawili hao walihakikishiana kuhusu upendo wao na kuahidi kusuluhisha mzozo wao na kuendelea kujenga familia pamoja.