Patanisho: Mimi si mhanyaji! Mwanamke amhakikishia mumewe ambaye hamuamini

Sina mwanaume mwengine, punguza hasira," alisema.

Muhtasari

• Fancy alisema kuwa mume wake, Steven Shatuma humsingizia kuwa na wanaume wengine.

• Mama huyo alisema kuwa Steven akimwona na mwanaume yeyote wakipiga gumzo yeye hufikiria kuwa wana uhusiano.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost, kitengo cha Patanisho, Fancy au Mama Kevo 25, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Steven Shatuma.

Fancy alisema kuwa uhusiano wake na mume wake umekuwa ukiyumbayumba kwa kuwa  mumewe amekuwa akimshuku kila mara kuwa na wanaume wengine.

Alisema kuwa Steven alimfungulia kibanda, ili aweze kujikimu na watoto wao watatu ila hakuwa mwenye amani kwenye biashara yake kwani mume wake alikuwa na kinyongo wakati wowote alipokuwa anaongea na wateja wanaume.

Mama huyo alisema kuwa Steven alikuwa anamsingizia kuwa na uhusiano na wateja wake wanaume punde tu alipomwona akizungumza nao.

"Hata aliniambia kuwa nisiwahi kuzungumza na mwanaume yeyote aliyekuwa anakuja kwenye kibanda kuuziwa au hata kumuuzia, ilifika wakati tukakosana kwa sababu ya kusingiziwa nikakusanya virago vyangu nikaenda kwa  mjomba wake," Fancy alisema.

Fancy alikuwa anataka kuhakikishia mume wake kuwa anampenda kwa dhati ili asiwe akimshuku kila mara.

Alisema kuwa mume wake alikuwa anawakorofisha wanaume wowote ambao walikuwa wanazungumza naye.

"Nilipokuwa kwa mjomba, siku moja, alinipigia usiku nikiwa nimelala, kufika asubui akanipigia nikamwambia nilikuwa nimelala kisha akaniambia kuwa nimerudisha tabia zangu za kuwa na wanaume nilizotoka nazo Nakuru ila si kweli," alieleza.

Alisema kuwa mume wake anapokuwa na fikra hizo huwa anakoma kufanya majukumu yake ya kuwa mzazi, hata kuwatumia watoto wao mahitaji.

Steven hakutaka kuzungumzia suala hilo hewani ila alisema kuwa hana mabaya kumwambia mke wake hayo na kuwa anampenda kwa dhati.

Alijieleza na kusema sababu yake ya kumkazia mkewe ni kuwa yuko mbali naye na hangetaka wanaume wengine kumkaribia.

"Nikikuambia hivyo huwa najaribu kukuzuia kufanya hivyo sikuambii kuwa hicho ndicho unachofanya. Huwa nakushtua ili usijaribu kufanya mambo mengine," Steven alisema.

Facy alimhakikishia mume wake kuwa nafasi yake bado ni ile ile na hajihusishi na wanaume wengine.

"Mimi sihanyi, usinifikirie mbaya kama unavyofanya. Nimetaka kupatanishwa nawe ili tuishi kwa amani, usirudi kuwa na fikira hizo tena,sina mwanaume mwengine, punguza hasira," alisema.