Patanisho: Jamaa aachwa kwa kumtania mkewe anajiua, adai alipata ajali na kuzimia siku 14

Vincent alidai kwamba kakake alimdanganya mkewe kuwa alikufa.

Muhtasari

•Mutunga alidai kuwa mkewe alibadilika na kusitisha uhusiano baada ya kudanganywa kwamba aliaga katika ajali iliyotokea mwezi Oktoba.

•"Alisema amemtuma kaka yake aendee kiberiti na akasema nisimtumie sms. Si wakati huo ndio akakufa," Angeline alisema.

Mtangazaji Ghost Mulee

Vincent Mutunga ,24, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Angeline Mulei ,20, ambaye alimtema baada ya kupata ajali.

Mutunga alidai kuwa mkewe alibadilika na kusitisha uhusiano baada ya kudanganywa kwamba aliaga katika ajali iliyotokea mwezi Oktoba.

"Miezi miwili iliyopita nilikuwa naenda kazi asubuhi kwa gari ya kazi. Nikiwa njiani nlipatana na mkosi kidogo kisha nikawa katika koma kwa siku 14. Kabla ya kuamka alikuwa amedanganywa na kaka yangu kwamba nimekufa," Vincent alisimulia.

Vincent alisema baada ya kuzinduka kutoka katika hali hiyo ya kukosa fahamu alimpigia simu mkewe lakini alisikika kuwa mkorofi na hakutaka chochote kuhusu yeye.

"Alichukua simu akaanza kuongea vibaya. Jumbe ambazo alikuwa ananitumia zilikuwa za kikorofi.Ni kama hanitaki.. Aliuliza kwani wafu huongea vipi," alisema.

"Kitambo angepiga simu hata nikiwa kazini. Alikuwa ananitumia sms. Sasa huwa anatuma moja moja tu."

Vincent alieleza kwamba Angeline ndiye aliyemueleza yote yalitokea wakati alipokuwa katika koma. Alisema kwamba hajazungumza na ndugu yake aliyedanganya kuhusu kifo chake tangu wakati huo.

"Wiki iliyopita nilimpigia, mazungumzo yake yako hivi hivi, ni kama hataki turudiane," alisema.

Angeline alipopigiwa simu alidai kwamba Vincent alimtania kuwa anataka kujitoa uhai na kumtaka asiwasiliane naye tena kwenye simu.

"Aliniambia mama yake ni mgonjwa na yeye ndio tegemeo. Alisema hata shangazi wake wana pesa lakini hawataki kusaidia, akasema anaskia maisha yake yamefika mwishoni. Aliniambia nisitext tena anakufa," alisema Angeline.

Aliongeza, "Alisema amemtuma kaka yake aendee kiberiti na akasema nisimtumie sms. Si wakati huo ndio akakufa."

Angeline alithibitisha kwamba baada ya kutuma ujumbe mwingine kwa kweli hakujibiwa. Baadaye kakake Vincent alimwambia kwamba baada ya kurudi nyumbanialimpata mpenziwe  huyo wake amejitia kitanzi.

"Kaka yake alirudi kwa nyumba akasema amepata Vinnie amejinyonga. Aliniambia Vinnie amechukuliwa amepelekwa mochari. Ilikuwa Ijumaa, Jumamosi aliniambia kwamba walipata barua ambapo Vinnie alisema kwamba alikuwa ameacha shilinhi laki saba kwa benki na zingine laki tatu kwa ajili ya mamake mgonjwa,"

Alisema kuwa aliarifiwa  mpenzi huyo angezikwa tarehe 2 Desemba, siku ambayo alikuwa akifanya mitihani yake.

"Singeweza kukosa mtihani. Nilimaliza mtihani nikaenda kwetu. Juzi juzi tu ndio aliniambia alipata ajali," alisema.

Huku akijitetea, Vincent alisisitiza kwamba kwa kweli alipata ajali na kuingia katika koma kwa siku kumi na nne.

Alidai kwamba alipata ajali kutokana na msongo wa mawazo uliomkumba kufuatia ugonjwa wa mama yake.

Angeline alisema kwamba yuko tayari kumpa Vincent nafasi nyingine licha ya utani ambao alimfanyia.

"Nakupenda na ndio maana nataka kukupatia nafasi ya pili," Angeline alisema.

Ghost alijitolea kufuatilia kwa maafisa wa polisi ili kubainisha kama kwa kweli alipata ajali.