Patanisho: "Mimi sina bibi!" Jamaa amruka mkewe hewani baada ya kunyakuliwa na mjane

Muhtasari

•Mercy alisema ndoa yao ya miaka miwili ilisambaratika mwezi Januari baada ya kumshuku mumewe kwa kutoka kimapenzi na mwanamke jirani.

•Mwanadada huyo alieleza kuwa mwanamke ambaye mumewe alikuwa anatoka kimapenzi naye  ni mjane. 

•Derrick alimkana Mercy huku akidai kuwa walikuwa washirika tu katika biashara ambayo walifunga.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, mwanadada aliyejitambulisha kama Mercy Nelima alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Derrick.

Mercy alisema ndoa yao ya miaka miwili ilisambaratika mwezi Januari baada ya kumshuku mumewe kwa kutoka kimapenzi na mwanamke jirani.

Alidai kuwa mumewe alikasirika na kumpiga wakati alipopiga hatua ya kumuuliza kuhusu madai hayo.

"Tulikuwa tunapendana lakini akaanza kusikiliza maneno ya baba na mama. Majirani wakaanza kuingilia pia. Nilisikia fununu kuwa ana mahusiano na mwanamke mwingine. Nilipomuuliza akanigombanisha na kunipiga," Mercy alisema.

Mwanadada huyo alieleza kuwa mwanamke ambaye mumewe alikuwa anatoka kimapenzi naye ni mjane. Alidai kuwa mumewe alikuwa anaenda kuonana naye kwake mara kwa mara.

"Nilisikia kutoka kwa majirani na marafiki nilipochunguza nikaanza kuona kama ni ukweli ndiposa nikamuuliza. Huyo mama alikuwa anamuita kila mara wanakaa kwa nyumba. Nilikuja kugundua, kuulizia akaanza kunichapa akisema mimi ni bibi yake," Alisema.

Derrick alisita kuchukua simu mara moja ila baada ya kushawishiwa na rafikiye akakubali kuzungumza na Patanisho.

Hata hivyo alimkana Mercy huku akidai kuwa walikuwa washirika tu katika biashara ambayo walifunga.

"Mimi sina bibi. Huyo tulimalizana kitambo. Tulimaliza biashara. Huyo alioleka ako kwake. Najua mahali penye ako," Alisema. 

Derrick aliashiria wazi kuwa hana nia ya kufufua mahusiano yake na Mercy na hata kukataa kushughulikia mtoto wao. 

"Fanya kazi yako. Shughulika na zako. Mimi sina shughuli na wewe. Tulifunga biashara na wewe. Huyo mtoto ata sijui kama ni wangu," Alimwambia Mercy.

Mercy alimhakikishia baba huyo wa mtoto wake kuwa bado anampenda ila akatishia kuchukua hatua kali baada ya kukataa kushughulikia mtoto.

"Tutakutane kwa ground. Najua tamsaidia," Alisema.