Patanisho: "Sina muda wa stress ya mapenzi!" Mwanadada azima juhudi za mumewe kuomba msamaha

Maina alibainisha kuwa tayari ameachana na mpango wa kando.

Muhtasari

•Maina alisema mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja mwezi juni 2021 kutokana na mambo ya mpango wa kando. 

•Catherine hakulegeza msimamo wake licha ya juhudi nyingi za Maina kujitetea.

Mtangazaji Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Edwin Maina ,22, kutoka Murang'a alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Catherine Muthoni.

Maina alisema mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja mwezi juni 2021 kutokana na mambo ya mpango wa kando. 

"Nilikuwa na mpango wa kando. Hakunipata, aliambiwa huko nje," alisema.

Aliongeza "Huwa anafanya kazi Thika, alikuwa anakuja mara mbili kwa mwezi. Sasa nampigia simu kisha ananiambia nirudi kwa huyo mke wangu. Najua hana mtu mwingine. Kuna mtu mwingine wanakaa naye ambaye ananiambia,"

Maina alibainisha kuwa tayari ameachana na mpango wa kando na amefanya maamuzi ya kuwa  na Bi Catherine.

Catherine alipopigiwa simu alisema hana kinyongo chochote dhidi ya mzazi huyo mwenzake ila akaweka wazi kuwa hawezi kurudiana naye. Alimwomba Maina kuendelea na maisha yake huku akibainisha kuwa yuko sawa.

"Nilikusamehe lakini hatuwezi kurudiana. Yale ambayo uliniambia yalitosha. Wakati ulisema uko na mpango wa kando nilifanya maamuzi. Wewe endelea na maisha yako na mimi niendelee yangu," alisema

Catherine hakulegeza msimamo wake licha ya juhudi nyingi za Maina kujitetea.

"Mimi niko sawa. Aendelee na maisha yake na mimi niendelee na yangu," alisema Catherine.

Huku akieleza sababu ya maamuzi yake, Catherine alifichua kwamba mumewe huyo wa zamani ndiye aliyemfichulia kuwa ana mpango wa kando.

"Yeye mwenyewe aliniambia. Alinipigia simu akaniambia tulikuwa wawili na amegundua kuna mmoja mzuri kuliko mwingine. Nilimwambia ni sawa aendelee na huyo mwingine. Nilimuuliza kwani huyo mwingine ana nini yenye sina," alisema.

Maina alijaribu kumsihi mama huyo wa mtoto wake akubali wakae chini pamoja wasuluhishe mzozo wao ila juhudi zake ziligonga mwamba.

 "Niko na mengi ya kufanya maishani. Sina wakati wa stress ya mapenzi.  Lazima nifanye kazi mtoto wangu akule. Sina wakati wa kukaa chini." alisema Catherine.