Patanisho:Mchungaji ampata mkewe akimcheza baada ya kupata maono

Simon alisema aliweza kumfumania mkewe baada ya kupata maono kuhusu mienendo yake.

Muhtasari

•Martha alikiri kuwa wakati mumewe aliporejea nyumbani, yeye na mpenzi wake walikuwa wameenda kujivinjari.

•Simon alisema yuko tayari kumkubali tena mkewe kurudi nyumbani mradi tu awe ametubu na kubadilisha tabia zake.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kitengo cha Patanisho, Martha (30)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Simon (35).

Martha alisema kuwa  mumewe alimfukuza nyumbani miezi mitatu iliyopita baada yake kutoka nje ya ndoa yao ya miaka mitatu. 

"Mume wangu alikuwa anakaa mjini. Hakuwa anarudi nyumbani. Kuna jamaa alikuwa ananikatia, nilimkataza lakini hakutaka kusikia," Martha alisimulia.

"Kwa vile mume wangu alikuwa mbali nikasema wacha nijaribu. Kumbe kujaribu ndio kushikwa! Mzee alinipigia simu akaniambia anakuja. Alipofika nyumbani alikuwa ananipigia simu sikuwa nashika. Aliuliza kwa nini sikuwa nashika simu nikajaribu kuficha," Alisema.

Martha alikiri kuwa wakati mumewe aliporejea nyumbani, yeye na mpenzi wake walikuwa wameenda kujivinjari.

"Watoto walikuwa wameenda date na mimi nikaenda date na huyo jamaa. Tulikula pamoja, tukakunywa lakini katika ile harakati ya kusoma katiba mashine ikalala. Niliporudi nyumbani mume wangu hakutaka kuongea na mimi. Aliniambia niende nyumbani. Mimi nampenda mume wangu sana. Ningependa kurudi tulee watoto"

Simon alipopigiwa simu alitaka kujua ikiwa mkewe tayari ameomba na kutubu kama alivyokuwa amemuelekeza.

Alisema kuwa yeye ni mchungaji na aliweza kumfumania mkewe baada ya kupata maono kuhusu mienendo yake.

"Mimi nilikusamehe. Nilikupatie muda wa kutubu.Unajua mimi sijawahi kuhanya hata siku moja," Simon alisema.

"Ni kitu yenye anafanyanga. Mimi ni mchungaji. Mimi huona kiroho. Nilimpigia simu nikamwambia kuna mambo anayofanya ambayo hayanifurahishi. Alikuwa anapinga. Vile alifika kwa nyumba nilimwambia aende akatubu.

Nilikuwa narudi nyumbani mara mbili kwa tatu. Wakati huo pekee ndio nilikuwa nimekaa mwezi mmoja bila kurudi kwa sababu nilikuwa na shughuli nyingi za maombi. Nilikuwa namuuliza anaongea na nani kwa simu alafu ananificha," Alisema.

Simon alisema yuko tayari kumkubali tena mkewe kurudi nyumbani mradi tu awe ametubu na kubadilisha tabia zake.

"Mimi nampenda Mungu. Huyo ni mke wangu. Kama anakiri amebadilika ni vizuri arudi watoto bado wako hapa. Shida ni arudi alafu hiyo pepo iwe ndani yake bado. Asiwahi kurudia. Akuwe mtu wa maombi," Alisema.

Wawili hao waliweza kuelewana na Simon akamwambia Martha kuwa yupo huru kurudi nyumbani leo.