'Nahitaji maombi' Ringtone Apoko afunga safari kuelekea Afrika Kusini kupokea matibabu zaidi

Apoko alifahamisha mashabiki wake kuwa safari yake ni kwa minajili ya matibabu na kuwasihi waendelee kumuombea.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alipakia picha kwenye ukurasa wake wa Instagram asubuhi ya Jumatano akiwa mahali ambapo palionekana kuwa uwanja wa ndege huku akionekana kana mwamba alikuwa anahudumiwa na mmoja wa wahudumu pale.

•Apoko alipokuwa katika mahakama ya Kibera wiki iliyopita kushuhudia mwanablogu Robert Alai akisomewa mashtaka alisema kuwa angefunga safari kuelekea Afrika Kusini kwa matibabu zaidi akidai kuwa hali yake ya afya haikuwa njema.

Image: INSTAGRAM//RINGTONE APOKO

Drama za mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko bado zinaendelea huku sasa akidai kuwa yuko safarini kuelekea Afrika Kusini kupata matibabu zaidi.

Mwanamuziki huyo alipakia picha kwenye ukurasa wake wa Instagram asubuhi ya Jumatano akiwa mahali ambapo palionekana kuwa uwanja wa ndege wa JKIA  huku ikionekana kana mwamba alikuwa anahudumiwa na mmoja wa wahudumu pale.

Mbele yake palikuwa na begi mbili kubwa zinazoashiria mtu kafunga safari ya mbali.

Apoko aliambatanisha picha hiyo na ujumbe wa kufahamisha mashabiki wake kuwa safari yake ni kwa minajili ya matibabu na kuwasihi waendelee kumuombea.

"Maombi yanahitajika kwa mwanamuziki wa nyimbo za injili mnayempenda anapoenda Afrika Kusini kupata matibabu" Apoko aliandika.

Mashabiki wake waliendelea kumtakia afueni ya haraka huku wengine wakitilia shaka maumivu anayodai kuwa yamekithiri.

Mwanamuziki huyo alipokuwa katika mahakama ya Kibera wiki iliyopita kushuhudia mwanablogu Robert Alai akisomewa mashtaka alisema kuwa angefunga safari kuelekea Afrika Kusini kwa matibabu zaidi akidai kuwa hali yake ya afya haikuwa njema.