"Acheni haraka ya kuwa mabundesko" Mike Sonko aonya vijana dhidi ya kujihusisha na biashara haramu ya 'Wash Wash'

Amewashauri vijana kuacha pupa ya kukimbilia utajiri akidai kuwa kwa mara nyingi biashara hizo haramu huhusisha hatari kubwa maishani

Muhtasari

•Kulingana na Sonko, mtu anapotumia njia haramu kupata mafanikio maishani ni rahisi sana kwake kurejea katika hali ya ufukara  ama zikawaletea matatizo baada ya kuwa kileleni kwa muda.

•Amesema kuwa mtu anapotumia njia fupi na rahisi kujipatia utajiri hawezi kubaki tajiri milele kwani ni rahisi sana kujipata umepoteza kila kitu ghafla.

•Sonko amefichua kwamba kunao watu wengi  ambao wamejaribu kumshawishi ajiunge na biashara haramu ya 'Wash Wash' akiahidiwa utajiri wa kupindukia.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amewatahadharisha vijana dhidi ya kukimbilia utajiri na mafanikio maishani.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, mwanasiasa huyo amewashauri vijana kuwa utajiri na mafanikio maishani hutokana na kazi kutia bidii kazini.

Kulingana na Sonko, mtu anapotumia njia haramu kupata mafanikio maishani ni rahisi sana kwake kurejea katika hali ya ufukara  ama zikawaletea matatizo baada ya kuwa kileleni kwa muda.

"Hizi deals za usiku kucha kisha unaanza kuendesha Porche Panama na huwezi kueleza namna unapata pesa zitawachimbia kaburi zenu mapema. Mafanikio matamu huwa na hadithi. Unaanza biashara, unajaribu na kuanguka mara kadhaa hadi biashara yenyewe inakufunza masomo muhimu kuhusu pesa" Sonko aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mfanyibiashara huyo amesema kwamba maisha hayana njia fupi  na lazima mtu apitie mashida mbalimbali ndiposa mwishowe aweze kupata mafanikio.

Amesema kuwa mtu anapotumia njia fupi na rahisi kujipatia utajiri hawezi kubaki tajiri milele kwani ni rahisi sana kujipata umepoteza kila kitu ghafla.

"Maisha hayana njia fupi, ndio maana kina baba zetu waliendesha magari kwa mara ya kwanza wakiwa na umri wa miaka 40 na 50. Uzoefu wa maisha hauna njia fupi, ndio maana kina babazetu walimaliza kujenga nyumba baada ya miaka mingi.

Ndoa haina njia fupi, lazima upitie matatizo. Lazima uijenge kwa kupitia kwa shida.

Hakuna kitu rahisi kupata, na kama siku moja utaamka ukiwa milionea basi jua huweza kaa sana pale kileleni. Hii biashara ya Wash Wash itawanufaisha kwa muda tu. Tunajua tu huwezi kaa pale kileleni mileleni" Amesema Sonko.

Mbunge, seneta na gavana huyo wa zamani amefichua kuwa kunao watu wengi  ambao wamejaribu kumshawishi ajiunge na biashara haramu ya 'Wash Wash' akiahidiwa utajiri wa kupindukia.

Sonko amewashauri vijana kuacha pupa ya kukimbilia utajiri akidai kuwa kwa mara nyingi biashara hizo haramu huhusisha hatari kubwa maishani.

"Lazima muelewe vitu mbili kuhusu biashara hizo. Mwanzo huwezi kudanganya 'samaki wakubwa' kwenye biashara. Unapofanyan hayo basi hawatasita kukupiga risasi. Pili huwezi washinda kiakili. Huwezi jua biashara zao za siri, wanakuangalia zaidi ya mama yako. Maisha gani hayop ambapo huna mahali pa kutumia pesa zako kwani  unachunguzwa. Kama si na 'samaki wakubwa' basi unapelelezwa na DCI. 

Acheni haraka ya kuwa mabundesko. Wakati wenu utafika. Angalia ukikua na utafurahia bila wengine kukuchunguza" Sonko amesema.

Siku za hivi karibuni biashara ya 'Wash Wash' imekuwa midomoni mwa Wakenya wengi na kwenye vyombo vya habari ikidaiwa kuna watu wengi mashuhuri ambao wanajihusisha nayo ili kujipatia utajiri wa haraka.