"Amapiano imeua Bongo Flava!" Eric Omondi alalamika

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama maishani amesema anasikitika sana kuona tukipoteza utambulisho na fahari yetu huku akiwaasihi wasanii wa Bongo kurejelea muziki asili na kuacha kuiga majirani.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amelalamikia kitendo cha wasanii wengi wa Afrika Mashariki kuiga mtindo wa muziki wa Amapiano.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Omondi amedai kwamba kwa sasa wasanii wengi katika kanda ya Afrika Mashariki  wamejitosa kwenye mtindo wa Amapiano, hatua ambayo imeathiri vibaya muziki uliosherehekewa zaidi wa Bongo Flava.

Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama maishani amesema anasikitika sana kuona tukipoteza utambulisho na fahari yetu huku akiwaasihi wasanii wa Bongo kurejelea muziki asili na kuacha kuiga majirani.

"Afrika Mashariki nimesikitishwa sana!!! Nawalilia watu wangu😥😥😥. Nina Huzuni Moyoni😥. Bongo flava imekuwa fahari ya Afrika Mashariki ila Kwa sasa imekufaa. Kila msanii wa Tanzania kwa sasa anaimba Amapiano. Tumepoteza utamaduni wetu, Tumeua chetu!!! Tumekaribisha, tumeiga, tumechukua tabia na mienendo ya jirani tukajisahau wenyewe😥😥😥. Tunapoteza utambulisho, fahari yetu!!! Naomba ndugu Zangu Wa BONGO Turejee kwa upesi kabla iwe tumechelewa!!! Wakenya wamelala, Wa Tanzania wamejipoteza. Mungu tuhurumie, turehemu🙏🙏😥😥" Aliandika Eric Omondi.

Amapiano ni mtindo wa muziki wa House ambao uliibuka nchini Afrika Kusini takriban mwongo mmoja uliopita.

Muziki huo umekuwa ukivuma kote Afrika na hata katika mataifa ya ughaibuni haswa siku za hivi majuzi. Wanamuziki kutoka mataifa mengine ikiwemo Tanzania na Kenya hivi majuzi wameonekana kuanza kuiga mtindo huo.