Diamond amsherehekea mwanawe Prince Nillan, adokeza kumwachia zana zake za muziki

Mtoto huyo wa Diamond na Zari anaadhimisha kutimiza miaka 7.

Muhtasari

•Prince Nillan ambaye ni mtoto wa pili wa wapenzi hao wa zamani anaadhimisha kutimiza miaka saba duniani.

•"Baba anakupenda Nee, kua nikupasie kijiti," alisema.

Image: INSTAGRAM// PRINCE NILLAN

Leo hii, Disemba 6, mtotowa  Diamond Platnumz na Zari Hassan, Prince Nillan anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Prince Nillan ambaye ni mtoto wa pili wa wapenzi hao wa zamani anaadhimisha kutimiza miaka saba duniani.

Diamond ametumia fursa hiyo kumsherehekea mwanawe na kumhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Mvulana wangu mtanashati alizaliwa leo. Mtoto wa mfalme, @princenillan," Alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Diamond aliambatanisha ujumbe huo na picha ya mtoto huyo  wake ambaye bila shaka ameendelea kukua kwa kasi kubwa

Katika ujumbe wake, staa huyo wa Bongo pia alidokeza kuhusu kuumwachia mwanawe uridhi wa muziki wake.

"Baba anakupenda Nee, kua nikupasie kijiti," alisema.

Kufikia kuchapishwa kwa makala haya, Zari  bado hakuwa amemwandikia mwanawe ujumbe wa siku ya kuzaliwa.

Nillan ni mtoto wa pili wa Diamond na mwanasoshalaiti wa Uganda Zari Hassan. Wapenzi hao wa zamani ambao wako na mtoto mwingine pamoja, Tiffah Dangote ambaye ana umri wa miaka saba.

Wazazi wenza hao walitengana mwezi Februari mwaka wa 2018 baada ya kuwa pamoja kwa takriban miaka minne.

Siku chache zilizopita Zari Hassan, ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini alitangaza kwamba atawapeleka watoto hao wake na Diamond nchini Tanzania ili kusherehekea Krismasi pamoja na familia ya baba yao.

Mwanasoshalaiti huyo alishiriki mazungumzo ya simu na Mama Dangote ambapo alimthibitishia kuhusu ziara hiyo ya Desemba.

Katika mazungumzo hayo, Zari alidokeza kuwa mpango wa kusherehekea sikukuu ya Krismasi nchini Tanzania ni uamuzi ambao alifanya pamoja na Diamond.

"Baba yao amesema wanakuja Krismasi. Bado tuko shule," Zari alimwambia Mama Dangote katika mazungumzo.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Zari Hassan na watoto wake kutembelea familia ya kina Diamond katika miaka ya hivi majuzi. Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 bado huwa anatembea nyumbani kwa mzazi huyo mwenzake licha ya wao kutengana takriban miaka minne iliyopita.

Mara nyingi anapozuru Tanzania, mama huyo wa watoto watano huwa ameandamana na watoto wake na Diamond, Tiffah na Nillan. Yeye na watoto hao wake wadogo wamehifadhi uhusiano mzuri na familia ya staa huyo wa Bongo licha ya tofauti zilizotokea hadi kuvunja mahusianoi yao ya muda mrefu.