Andrew Kibe afichua kura ndogo alizopata alipowania Ubunge Lang'ata

"Tafadhali, kabla mniongeleshe. Wekeni heshima kwenye jina langu," alisema.

Muhtasari

•Kibe aliwania kiti cha ubunge cha Lang'ata kwa tikiti ya chama cha UDF lakini  akalambishwa sakafu vibaya.

•Kibe alisema alikuwa tayari sana kwa kiti hicho cha kisiasa kabla ya ndoto yake kuangamizwa siku ya uchaguzi.

alipoenda kuchukua cheti cha uteuzi katika ofisi za IEBC mwaka wa 2013.
Andrew Kibe alipoenda kuchukua cheti cha uteuzi katika ofisi za IEBC mwaka wa 2013.
Image: HISANI

Mtengenezaji Maudhui mashuhuri wa Kenya, Andew Kibe Mburu amesimulia kuhusu safari yake fupi ya kisiasa.

Katika uchaguzi wa 2013, mtangazaji huyo wa zamani aliwania kiti cha ubunge cha Lang'ata kwa tikiti ya chama cha UDF lakini  akalambishwa sakafu vibaya.

Akizungumza katika mojawapo ya video zake, alisema alikuwa tayari sana kwa kiti hicho cha kisiasa kabla ya ndoto yake kuangamizwa siku ya uchaguzi.

"Nilikuwa tayari sana. Nilipata, kama sijakosea, labda 1400. Unaweza kufanya nini na 1400 kwa sarafu yoyote," alisema.

Mtumbuizaji huyo ambaye kwa sasa anaishi Marekani alionyesha baadhi ya mabango ya kampeni aliyotumia kujipigia debe mwongo mmoja uliopita.

Pia alionyesha cheti chake cha uteuzi wa UDF ambacho kilimuidhinisha kuwania kiti cha ubunge wa Lang'ata kwa tikiti ya chama hicho.

"Tafadhali, kabla mniongeleshe. Weka heshima kwenye jina langu. Hii ni siku ambayo nilikuwa naenda kuchukua cheti changu kwa IEBC," Kibe alisema kuhusu picha iliyomuonyesha akiwa amevalia suti na kitambaa cha UDF.

Takriban muongo mmoja uliopita, Andrew Kibe alitaka kuchukua nafasi ya Raila Odinga kama Mbunge wa eneo la Langa’ta, kaunti ya Nairobi lakini akapoteza kwa Joash Odiambo Olum wa chama cha ODM. Kabla ya hapo, Raila alikuwa mbunge wa Lang’ata  (wakati huo ikijumuisha Lang'ata na Kibera)  kwa zaidi ya miaka 20.

Katika uchaguzi huyo, Olum alimshinda aliyekuwa mbunge wa eneo hilo kati ya 2017-2022, Nixon Korir, kwa kura 7,654. Korir aliwani kwa tikiti ya URP na kupata kura 17,740 huku Olum akishinda kwa 25,394.

Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2013, Andrew Kibe hakujaribu tena kuwania kiti hicho ambacho kwa sasa kinakaliwa na aliyekuwa mtangazaji Phelix Odiwour almaarufu Jalang'o wa chama cha ODM.