Jinsi King Kaka alivyomzuia shabiki kujitoa uhai

Shabiki huyo alikiri kuwa alijiskia bora zaidi baada ya kuskiliza wimbo wa rapa huyo.

Muhtasari

•Shabiki mmoja wa King Kak alikiri kwamba wimbo wa rapa huyo  'Atanishindia' ulimsaidia kuondoa mawazo ya kujiua.

•Kwenye maelezo ya ujumbe huo, King Kaka aliwatakia afueni watu wote ambao wanapitia hali na wakati mgumu.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwimbaji wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu King Kaka amefichua ujumbe maalum wa simu kutoka kwa shabiki wake mmoja  ambaye alikuwa amekumbwa na mawazo ya kujitoa uhai.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, King Kaka alionyesha ujumbe wa shabiki wake ambaye  alikiri kwamba wimbo mpya wa rapa huyo akiwashirikisha Watendawili,  'Atanishindia' ulisaidia kuondoa mawazo yake ya kujiua.

Shabiki huyo ambaye hakufichuliwa alisema kwamba alijiskia bora zaidi baada ya kusikiliza maneno ya wimbo huo.

"Habari King, Atanishindia ni wimbo mzuri sana kwa roho, jana nilikuwa na mawazo ya kuitoa uhai lakini baada ya kusikiliza kibao hiki moto tena, najihisi mzuri, Hata nilijipata nikiandika vesi hapo," shabiki huyo alisema.

Kwenye maelezo ya ujumbe huo, King Kaka aliwatakia afueni watu wote ambao wanapitia hali na wakati mgumu.

"Huenda tunapitia nyakati na hali ngumu, naomba upate amani na suluhu katika jambo lolote unalopitia," aliandika.

Wimbo 'Atanishindia' ni miongoni mwa nyimbo za injili ambazo mwanamuziki huyo mahiri ameachia baada ya kupona ugonjwa wa kutisha ambao alipambana nao kwa miezi kadhaa mwaka wa 2021. 

Wakati akizungumza kwenye mahojiano na mwanavlogu Oga Obinna mwezi Januari, rapa huyo alifichua kwamba aliapa kutengeneza albamu ya nyimbo za injili kufuatia uponyaji wake wa kiajabu.

King Kaka alibainisha kuwa Mungu alihusika katika uponyaji wake wa kimuujiza huku akieleza kwamba amekuwa naye daima.

"Mimi huwa naamka na kitu cha kwanza ni kumwambia Mungu asante, kila asubuhi," alisema.

Kaka alisema uponyaji wake ulikuwa wa ajabu kwani wahudumu wa afya katika hospitali aliyokuwa amelazwa walithibitisha kuwa si watu wengi wanaotoka humo wakiwa hai baada ya kulazwa katika hali mbaya kama yeye.

King Kaka alifichua kwamba mchakato wa uponyaji wake ulianza usiku mmoja wakati bado akiwa amelazwa katika hospitali ambapo alianza kuona mambo yasiyo ya kawaida mwendo wa saa tisa usiku.

"Nilianza kuona vitu sijui. Nilianza kuona mwangaza, nikaona giza. Niliona ni wakati wangu wa kuishia. Niliambia Mungu kama wakati wangu niko tayari. Huwa inafika mahali hata unakubali kifo," alisimulia.

Alisema baada ya kufichuliwa mambo ya ajabu alimuomba Mungu na kufanya amani naye kwani alihisi anakaribia kufa.

Kiajabu, asubuhi iliyofuata alipata kifungua kinywa kwa mara ya kwanza baada ya siku tano hivi. Pia alikunywa supu baadaye.

"Hivyo ndivyo nilianza kula. Baada ya siku tatu, nne hivi nilikuwa natembea huko hospitali," alisema

Aliruhusiwa kuenda nyumbani siku tano baada kupata ufunuo wa ajabu usiku.

King Kaka alifichua kwamba uhusiano wake na Mungu umekuwa mzuri kwa miaka mingi ya maisha yake.