Marioo, Chino Kidd waomboleza kwa uchungu baada ya ajali mbaya kumuua mwenzao

Msanii Chino Kidd ameahidi kuendelea kumtunza mtoto wa marehemu ili kutimiza matakwa yake.

Muhtasari

•Chino amefichua kuwa marehemu Nabeel alikuwa akiweka juhudi kubwa katika kazi yake ili kumpa malezi mazuri mtoto wake ambaye sasa amemuacha.

•Staa wa Bongo Marioo pia amemuomboleza marehemu katika ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Instagram.

Chino Kidd, Marehemu Nabeel, Marioo
Image: INSTAGRAM

Staa wa Amapiano kutoka Tanzania, Chino Kidd hatimaye amevunja ukimya baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani iliyochukua maisha ya mmoja wa wenzake.

Katika taarifa yake Jumapili alasiri, Chino ambaye alinusurika kwenye ajali hiyo mbaya ya barabarani iliyohusisha gari lao aina ya Toyota Alphard na lori la mafuta siku ya Jumatatu mchana aliomboleza rafiki yake Nabeel ambaye kwa bahati mbaya alipoteza maisha Jumapili asubuhi.

Nabeel ndiye aliyekuwa dereva wa Toyota Alphard iliyopata ajali ikiwa imembeba Chino Kidd na wenzake kuelekea kwenye hafla  katika mkoa wa Tanga.

“Daah, mtu wangu siwezi kuongea sana ila naamini Mwenyezi Mungu atakuweka sehemu salama na kuzidiwa kukuombea sana,” Chinno Kidd alimuomboleza marehemu Nabeel kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa msanii huyo wa Bad Nation kuzungumza hadharani baada ya kuhusika katika ajali hiyo iliyowatia wasiwasi mashabiki wa muziki wa bongo fleva.

Katika maelezo yake, mwimbaji huyo wa Bongo Amapiano alifichua kuwa marehemu Nabeel alikuwa akiweka juhudi kubwa katika kazi yake ili kumpa malezi mazuri mtoto wake ambaye sasa amemuacha. Chino hata hivyo ameahidi kuendelea kumtunza mtoto huyo ili kutimiza matakwa ya marehemu.

“Ndoto yako kubwa iliyosababisha mpaka tukapanga mipango mingi ilikua ni mtoto wako kipenzi uliyemuacha. Nakuahidi hatapata shida kabisa ikiwa bado nipo hai. Pumzika salama mwanangu,” Chino Kidd aliomboleza.

Marehemu Nabeel alikuwa akifanya kazi na lebo ya muziki ya Bad Nation inayomilikiwa na staa wa bongofleva Omary Mwanga almaarufu Marioo.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Mi Amor’ pia amemuomboleza marehemu katika ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Instagram.

"Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea," Marioo aliandika chini ya picha ya Nabeel ambayo aliiweka kwenye ukurasa wake.

Mastaa wengi wa bongo fleva pia wameendelea kumuomboleza marehemu Nabeel na kuwafariji watu wake wa karibu wakiwemo wenzake katika Bad Nation.

Nabeel alifariki kufuatia ajali mbaya iliyotoea siku ya Jumamosi ambayo ilimhusisha msanii Chino Kidd na kundi lake la muziki.

Chino Kidd na wenzake kadhaa walikuwa wakielekea katika mkoa wa Tanga kwa ajili ya shoo wakati gari aina ya Alphard nyeusi walilokuwa wamepanda, na ambalo liliendeshwa na Nabeel liligongana na lori la mafuta ya petroli.

Ajali hiyo inaripotiwa kutokea katika eneo la Kabuku Jumamosi mchana ambapo waathiriwa kadhaa wanaripotiwa kupata majeraha mabaya.

Mtayarishaji wa muziki kutoka Tanzania Abbah Process alithibitisha kifo cha Nabeel Jumapili asubuhi alipokuwa akimuomboleza.

“Rest in peace brother, tumepoteza mwanafamilia mmoja aliyekuwa kwenye ajali ya jana (Jumamosi). Mungu amkumbatie katika mikono yake yenye upendo na ampe amani ya milele. Milele mioyoni mwetu,” Abbah Process aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.