Nuru Okanga azungumza baada ya kujiunga na Sekondari ya kutwa licha ya kutamani Lenana na Alliance

Pia alimsihi mkuu wa shule hiyo kuwa anamwachilia saa mbili kabla ya wanafunzi wengine.

Muhtasari

•Okanga alifichua habari kuhusu kujiunga kwake na shule ya upili Jumanne kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo alisherehekea hatua yake hiyo mpya.

•Japo alikataa kufichua jina la shule ya upili aliyojiunga nayo, alibainisha kuwa ni shule ya kutwa ambayo itamwezesha kusawazisha kati ya elimu yake na familia.

Image: FACEBOOK// NURU MALOBA OKANGA

Shabiki sugu wa chama cha ODM na mfuasi mkuu wa kinara wa chama hicho Raila Odinga, Bw Nuru Maloba Okanga anaonekana hatimaye kujiunga na shule ya upili baada ya kufanya mtihani wa KCPE mwaka jana.

Okanga ambaye anafahamika kwa kuzungumza siasa sana katika kipindi maarufu cha ‘Bunge la Mwanachi’ alifichua habari kuhusu kujiunga kwake na shule ya upili Jumanne kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo alisherehekea hatua yake hiyo mpya.

Alishiriki picha yake akiwa amebeba begi na akiwa amevalia sare za shule.

"Mungu wa Okanga ametenda tena," Okanga aliandika chini ya picha hiyo aliyochapisha.

Wakati akiwahutubia Wakenya kupitia video, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 32 alisisitiza kwamba aliamua kujiunga tena na shule na kukamilisha masomo yake ili kuwania kiti 2027.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaomba Wakenya, wanafunzi wenzake na walimu kumuunga mkono anapoanza safari ya miaka minne ya shule ya upili.

“Naomba wanafunzi wenzangu tuhakikishe kwamba matokeo mazuri yametoka kwa shule hii. Na yatatoka kama sisi wanafunzi tutatia bidii na masomo,” alisema.

Japo alikataa kufichua jina la shule ya upili aliyojiunga nayo, alibainisha kuwa ni shule ya kutwa ambayo itamwezesha kusawazisha kati ya elimu yake na familia.

“Mimi nataka mashabiki wangu wajue niko shule. Kama mnavyojua, niko na uhasama na Ruto, na pia waziri wa elimu hayuko na mimi vizuri. Kwa hivyo mjue tu niko shule, nitafocus na hiyo shule, nitafocus na masomo. Mwalimu mkuu amesema nifiche mtoto wa kizungu. Mashabiki wangu waelewe mimi ni mwanafunzi,” Okanga alisema.

Aliongeza, “Nimeamua kwenda shule ya kutwa kwa kuwa majukumu ya familia ni lazima tushikilie. Tunasoma, na pia familia iko hapo. Nimeamua kwenda shule ya kutwa ili nihakikishe kwamba familia yangu isiharibike mahali popote. Tutang’ang’ana.”

Pia alimsihi mkuu wa shule hiyo kuwa anamwachilia saa mbili kabla ya wanafunzi wengine ili aendelee na kazi yake ya siasa katika Bunge la Mwananchi.

“Bibi yangu hana maneno. Pia atanisapoti kimasomo kwa sababu yeye ni mtu wa kidato cha nne. Tulizungumza na yeye akasema nijiunge na shule tusaidiana. Mke wangu hana shida, ni ile tu atakuwa ananimiss mchana,” alisema.

Pia alimwomba kiongozi wa ODM Raila Odinga kumuunga mkono katika safari yake mpya.

Awali, alidokeza kuwa anatamani sana kujiunga na Shule ya kitaifa ya Lenana au Alliance kwa masomo yake ya shule ya upili.