"Alinitongoza nikamkataa" Ringtone Apoko azungumzia uhusiano wake na mwanasoshalaiti Huddah Monroe

Muhtasari

•Alisema Huddah alikuwa anammezea mate sana kiasi cha kwamba angemlilia ili kupata huruma yake ila yeye hakumtaka.

•Ringtone alisema ingawa Huddah ni malkia mrembo hajahitimu kuwa mchumba wake kwa kuwa  imani yao hailingani.

•Aliweka wazi kwamba hataki mwanamke mrembo zaidi kwa kuwa anahofia kusumbuliwa sana.

Huddah Monroe, Ringtone Apoko
Huddah Monroe, Ringtone Apoko
Image: HISANI

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko ametilia shaka matamshi ya mwanasoshalaiti Huddah Monroe kwamba hakuna mwanamume yeyote wa Kenya aliyehitimu kuwa mchumba wake.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mwanamuziki huyo aliyezingirwa na drama si haba alisema kulingana na jinsi anavyomfahamu Huddah, hastahili kuwa anatoa matamshi kama yale.

Apoko alisema amemfahamu Huddah kwa miaka mingi na hapo zamani mwanasoshalaiti huyo alikuwa anammezea mate sana kiasi cha kwamba angemlilia ili kupata huruma yake ila yeye hakumtaka.

"Tumekuwa na safari refu sana ya maisha na Huddah Monroe.Tunajuana sana kwa vilemba.Hawezi sema hivo. Tumejuana miaka mingi. Ametoka mbali. Labda alikuwa anatafuta kiki ama alikuwa amelewa, huwa anakunywa sana msimhukumu. Hawezi sema mimi sio mtanashati na alikuwa ananililia kitambo, mimi ndio nilimkataa. Alikuwa  ananililia na kunisumbua sana eti ananitaka nikamkataa" Apoko alisema.

Mwimbaji huyo alidai kwamba Huddah alijaribu sana kumtongoza kwa njia zote ila juhudi zake zote zikaangulia patupu kwani yeye hakumtaka.

Ringtone alisema ingawa Huddah ni malkia mrembo hajahitimu kuwa mchumba wake kwa kuwa  imani yao hailingani.

"Alinitongoza nikakataa. Nilimwambia lazima aokoke ndivyo tuweze tuzungumzia mambo mengine. Ni msupu. Yeye ni mmoja wa wanawake warembo zaidi barani Afrika. Hata hivyo hawezani nami kwa kuwa lazima aokoke, atubu dhambi na amkiri Yesu. Hapo ndipo tulikosania. Nilimkataa kabisa" Apoko alisema.

Kando na suala la imani, Ringtone alisema sababu yake nyingine kumkataa Huddah ni kwa kuwa yeye ni mrembo kupindukia.

Ameweka wazi kwamba hataki mwanamke mrembo zaidi kwa kuwa anahofia kusumbuliwa sana.

"Nataka msichana anaomba masaa saba, anaweza kunizalia watoto saba na anayeogopa Mungu. Urembo uko kwa roho. Hao wasichana warembo kama Huddah siwataki" Apoko alisema.

Mwanamuziki huyo amesisitiza kwamba angali anaendelea kutafuta mwanamke atakayekidhi matakwa yake kwa mchumba.