"Waliofikiria siasa ni kila kitu ni bure kabisa!" Sonko ajigamba kuhusu maendeleo baada ya kutimuliwa siasani

Muhtasari

•Hivi majuzi mwanasiasa huyo alifungua kilabu kubwa ya kifahari jijini Mombasa inayotambulika kama VIP Volume Club. 

•Mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na drama amewashauri watu kuendelea kuwa na imani na kumuomba Mungu sana.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amejivunia maendeleo yake baada ya kutimuliwa siasani
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amejivunia maendeleo yake baada ya kutimuliwa siasani
Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameonekana kujivunia maendeleo yake baada ya kutimuliwa kutoka siasani mnamo takriban miaka miwili iliyopita.

Tangu kuondolewa kwake madarakani mnamo mwaka wa 2020, Sonko amejitosa  katika kazi mbalimbali mbali na siasa ikiwemo biashara.

Hivi majuzi mwanasiasa huyo alifungua kilabu kubwa ya kifahari jijini Mombasa inayotambulika kama VIP Volume Club. 

Katika ukurasa wake wa Facebook, mwanasiasa huyo alipakia video na picha zilizoonyesha akifanya kazi katika kilabu hiyo yake na kujivinjari pamoja na wateja.

Sonko aliendelea kueleza kwamba kutimuliwa kwake siasani kulikuwa tu kuvunjika kwa mwiko wala hakukumaanisha mwisho wa mapishi.

"Waliofikiria siasa ni kila kitu ni buree kabisa. Kazi ni kazi hebu oneni jinsi Mungu alivyo mwaminifu. Yani shetani akifunga mlango mmoja, Mungu anafungua mlango mwingine mara moja na maisha yanaendelea kama kawaida" Sonko aliandika chini ya video na picha zilizoonyesha akiwa kwenye kazi yake mpya.

Those who thought politics ni kila kitu ni buree kabisa. Kazi ni kazi hebu oneni how God is faithful. Yani the devil...

Posted by Mike Sonko. on Sunday, February 6, 2022

Mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na drama amewashauri watu kuendelea kuwa na imani na kumuomba Mungu. Vile vile aliwashukuru wateja wa kilabu yake mpya.

Sonko alitimuliwa ofisini kufuatia madai ya matumizi mabaya ya afisi ya gavana. Kwa sasa kiti alichokuwa amekalia kimeridhiwa na aliyekuwa naibu wake Anne Kananu.