Mapenzi tight! Bahati amnunulia mkewe Diana Marua shamba kama zawadi ya Valentines

Muhtasari

•Bahati alisema kwamba kwa muda mrefu mama huyo wa watoto wake amekuwa akitamani kumiliki shamba ambapo anaweza kujenga nyumba ya ndoto zake.

•Alipatia kipenzi hicho chake idhini ya kufanya chochote atakachotamani kufanya na kipande kile cha shamba.

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Huku siku ya wapendanao ya Valentines ikiwa inawadia kwa kasi, mwanamuziki mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu kama Bahati amemsurprise mpenzi wake Diana Marua na zawadi ya shamba.

Bahati alisema kwamba kwa muda mrefu mama huyo wa watoto wake amekuwa akitamani kumiliki shamba ambapo anaweza kujenga nyumba ya ndoto zake.

Alisema kuwa ameafikia kufanikisha ndoto ya mpenzi wake ili kuashiria upendo mkubwa alio nao kwake na kumuonyesha kuwa alinyakuliwa na mume bora.

"Nilichugua hili kama zawadi ya kwanza kwa sababu kwa muda mrefu hii imekuwa ndoto yako. Ni kitu ambacho umetamani kuwa nacho." Bahati alisema huku akimkabidhi mpenzi wake hatimikili ya shamba.

Baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo, Diana aliwezwa na hisia na hata kububujikwa na machozi mengi ya furaha.

Bahati alipatia kipenzi hicho chake idhini ya kufanya chochote atakachotamani kufanya na kipande kile cha shamba.

"Unaweza kujenga nyumba ya ndoto yako kwa shamba hili. Unaweza ukatengeneza bwawa la kuogelea. Unaweza kujenga vitu vyote vya ndoto zako hapo" Bahati alimwambia Diana.

Diana alimshukuru mpenziwe na kumwombea baraka tele huku akimhakikishia kuhusu mapenzi aliyo nayo kwake.

"Ndio nimeanza tu. Natamani ungejua yale niliyokuwekea katika siku nne zijazo mpaka siku ya Valentines" Alisema Bahati.

Hapo awali Bahati alikuwa ameahidi kumpa mpenzi wake zawadi tano kubwa katika msimu huu wa Valentines.

Diana vilevile ameapa kwamba mwaka huu lazima ajikakamue kumsurprise mumewe kutokana na mahaba ambayo ameendelea kumuonyesha.