Butita adai Sosuun na Vivianne walifeli, "wangenitafuta nichore"

Muhtasari

• Alitamani wangemtafuta ili awandalie igizo hilo kwa minajili ya kutokea kwa njia ya kiasili kabisa na wala si maigizo kama ambavyo wengi wameichukulia video hiyo.

Eddie Butita
Eddie Butita
Image: Facebook

Mchekeshaji na muongozaji wa filamu za humu nchini Eddie Butita anaashiria kutofurahishwa kwake na kitendo kinachosemekana kilikuwa cha kuigiza ambapo msanii Sosuun anaonekana akimshambulia msanii mwenziwe Vivianne.

Katika video hiyo ambayo Sosuun alimtaka mtu waliyeandamana naye kumfuata Vivianne katika studio ambapo alikuwa akifanya muziki, msanii huyo anaonekana akirukia na kumparura Vivianne huku akimfokea kwa kumtukana mitandaoni.

Lakini kisa kizima kinaonekana kama tukio ambalo lilitayarishwa katika maandishi na kuigizwa ili ionekane kwamba wawili hao wana ugomvi mkali unaopelekea kutafutana na kushambuliana si tu kwa maneno bali mpaka kwa vitendo pia.

Baada ya video hiyo kusambazwa kwenye mitandaoni ya kijamii, Muongozaji wa filamu kama hizo za kuigiza Eddie Butita alidakia hapo na kutoa wazo lake, huku akihisi kama ni kitendo kilichoandaliwa basi walifeli sana.

Alitamani wangemtafuta ili awandalie igizo hilo kwa minajili ya kutokea kwa njia ya kiasili kabisa na wala si maigizo kama ambavyo wengi wameichukulia video hiyo.

“Wangenitafuta nichore hii kitu fiti, sasa ona inakaa play ya high school,” aliandika Eddie Butita.

Katika video hiyo, Vivianne alisikika akifoka kwamba Sosuun amemharibia muda wake wa mazoezi katika studio na angemchukulia hatua lakini baadae akandika kwenye Facebook kwamba hatafanya hivo na kudokeza kwamba collabo yao ingetoka Alhamis mchana.

Ilikuwa ni kiki tu tangu mwanzo walipoanza kutupiana maneno kwamba Sosuun amekawia bila ya kuachia muziki huku naye akimjibu Vivianne kwamba amekawia kumzalia bwanake mtoto.