"Anapenda Mungu na Dhahabu" Harmonize afichua sababu ya kumnunulia Kajala cheni ya dhahabu

Muhtasari

• Katika siku za hivi karibuni, Harmonize amekuwa akifanya vitu vya kiajabu ajabu kwa ajili ya kutaka kurudiana na muigizaji huyo mkongwe wa filamu za bongo.

Harmonize, Kajala fridah masanja
Harmonize, Kajala fridah masanja
Image: Instagram

Moyo wa msanii na mkurugenzi mkuu wa rekodi lebo ya Konde Music Worldwide, Harmonize umekataa kabisa kusonga mbele kutoka himaya ya mwanamama Fridah Kajala.

Katika siku za hivi karibuni, Harmonize amekuwa akifanya vitu vya kiajabu ajabu kwa ajili ya kutaka kurudiana na muigizaji huyo mkongwe wa filamu za bongo.

Baada ya kulipia bango kubwa lenye picha ya pamoja kubandikwa katika moja ya barabara jijini Dar es Salaam bila majibu, Harmonize ameona bado haitoshi na kupiga hatua ya kiume zaidi ambapo amemnunulia Kajala cheni ya shingoni yenye thamani ya takribani robo milioni pesa za kenya, kwa maana ya 250K ambazo ni sawa na milioni 5 za Jamhuri ya Tanzania.

Harmonize ameipakia kwenye instastories zake cheni hiyo ya dhahabu na kusema kwamba ameamua kuifanya kuwa zawadi kwa Kajala kwa sababu anaamini mwanamama huyo anapenda Mungu na Dhahabu.

“Anapenda Mungu na Dhahabu. Hii ni hatari, jamani mtu amwambie akubali kunirudia. Ni jambo la kimboleambolea kutumia pesa zako kwa mtu unayempenda. Tafadhali mtu amwambie aniondoe kwenye listi ya block, Instagram,” aliandika Harmonize.