MCA Tricky afunguka kuhusu maisha yake kama Chokoraa

Tricky alifichua kwamba aliishi mitaani kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Muhtasari

•MCA Tricky ameeleza kwamba hali yake haikuwa imefikia kama ile ya vijana wanaonusa gundi mitaani.

•Pia alifichua kwamba aliwahi kuishi mahali ambapo alikuwa analipa kodi ya shilingi hamsini tu kwa usiku mmoja.

Image: INSTAGRAM// MCA TRICKY

Mchekeshaji Francis Munyao almaarufu MCA Tricky ameweka wazi kwamba ni kweli aliwahi kuishi mitaani.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Tricky alifichua kwamba aliishi mitaani kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Msanii huyo hata hivyo alieleza kuwa hali yake haikuwa imefikia kama ile ya vijana wanaonusa gundi mitaani.

"Kuna wakati nilikuwa mitaani. Ni hatua ya maisha tu. Maisha hubadilika. Unaweza kujipata kule kwa miezi. Lakini ilitokea kwa kipindi kifupi, haikuwa zaidi ya mwaka," Tricky alieleza.

 "Bila shaka kwangu sikuwa kama hao wa kuvuta glue. Watu wakifikiria kuhusu chokoraa wanaona lazima uwe kama hao. Kuna watu ambao wanafanya kazi za maana lakini hawezi kumudu kodi," Aliongeza.

Mchekeshaji huyo pia alifichua kuwa aliwahi kuishi mahali ambapo alikuwa analipa kodi ya shilingi hamsini tu kwa usiku mmoja.

"50 bob tumelipa sana pale Ngara na watu wengi. Hata wasee wengine huamka hapo na suti wakiwa wamebeba stakabadhi zao wanaenda kutafuta kazi.. maisha ya mitaani haimaanishi kuwa mchafu au kuvuta glue, unaweza kuwa sawa lakini huna mahitaji ya msingi," Alisema

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata umaarufu mkubwa wakati alijiunga na Churchill Show takriban miaka sita iliyopita.

Tricky alisisimua Wakenya wengi kwa vichekesho vyake ambavyo mara nyingi viliangazia maisha ya mitaani.

Hata hivyo ameweka wazi kwamba hakuwa akitafuta huruma kwa kusimulia hadithi za maisha ya mtaani jukwaani.

MCA Tricky ni mhitimu wa uhandisi lakini hata hivyo alichagua kufuata taaluma yake ya uchekeshaji. Kando na uchekeshaji na uhandisi yeye pia ni mtangazaji huku akiwa amefanya kazi katika vyombo kadhaa vya habari.