Ripoti: Watoto 5 wa familia moja walifariki kwa kula ugali na maziwa ya sumu

Vifo hivyo vilitokea katika Kijiji cha Mswakini Chini, wilayani hapa Mkoa wa Arusha, Tanzania.

Muhtasari

• Wazazi wa watoto hao walikuwa washukiwa wa kwanza na kutiwa nguvuni ambapo mpaka mazishi ya wanao walikuwa kizuizini.

Miili ya watoto watano wa familia moja waliofariki kwa kula sumu ikiagwa
Miili ya watoto watano wa familia moja waliofariki kwa kula sumu ikiagwa
Image: YouTube Screengrab

Wiki iliyopita, mitandao ya kijamii ilisikitishwa na taarifa kuhusu watoto watano wa familia moja waliofariki kutokana na kile uchunguzi wa kimatibabu katika maabara ya serikali ya Tanzania ulisema kwamba walikula au kunywa kitu chenye sumu kali.

 

Siku chache baada ya kuzikwa katika kaburi la pamoja, hatimaye uchunguzi umetoka na inasikitisha kwamba chakula walichokula chenye sumu ni ugali na maziwa, chakula ambacho kiliandaliwa na wazazi wa watoto hao marehemu.

 

“Chakula cha mwisho walichokula watoto watano wa familia moja kinachodaiwa kuwapotezea maisha Kijiji cha Mswakini Chini, wilayani hapa Mkoa wa Arusha kimeelezwa kuwa ni ugali na maziwa ulioandaliwa nyumbani na wazazi wao,” taarifa kutoka vyombo vya habari nchini humo ilisoma.

Kulingana na taarifa, watoto hao marehemu walikula chakula hicho cha sumu mnamo Julai tarehe moja kabla ya kuanza kulalamika maumivu makali ya tumbo pamoja na kujaa gesi.

 

Watoto watatu waliofariki dunia Julai 20 na mmoja juzi wamezikwa jana. Mtoto aliyefariki dunia Julai 5 alizikwa wiki iliyopita.

Baba mdogo wa watoto hao, Kirong’a Mollel alisema Julai Mosi mmoja kati yao alionekana kuzidiwa zaidi hivyo alichukuliwa na kupelekwa hospitali binafsi, kabla ya kufariki dunia.

 

“Hawa wengine nao, wakaanza kuvimba tumbo na wakapatiwa matibabu nyumbani na baada ya hali kuwa mbaya, walipelekwa Hospitali ya Jeshi Monduli (TMA), walipotibiwa walipata nafuu, lakini wakati wanarudi nyumbani, hali ilibadilika, wakapelekwa Hospitali ya Mkoa Mount Meru ambako walifariki dunia,” alisema Mollel.

 

Hata hivyo, alisema ugali na maziwa ni chakula walichokuwa wakila siku zote wakitoka shuleni na kuchunga mifugo.

“Hatuna chakula kingine pale nyumbani, ni ugali na maziwa tu, ndiyo maana tunaomba uchunguzi zaidi ufanyike kujua hiyo sumu ilitoka wapi,” alidai Mollel kulingana na taarifa kwenye vyombo vya habari nchini humo.

Mwanafamilia mwingine, Leseno Mollel alisema watoto hao walikuwa wakiishi na wazazi wao pekee na ni familia ya mke na mume mmoja na hawajawahi kushuhudia mgogoro ambao labda wangeweza kuuhusisha na vifo hivyo. Alisema baba wa watoto hao, Nyangusi Mollel na mke wake, Nandoye Nyangusi walikuwa na watoto saba na mmoja bado ananyonya ambaye aliponea kifo kile chenye utata mkubwa.

 

Mpaka waakti mazishi ya watoto hao yanafanyika, wazazi wote wawili walikuwa mikononi mwa vyombo vya usalama na hawakuweza kupewa nafasi ya kuhudhuria mazishi na kuwapa buriani, kwani walidhaniwa kuwa washukiwa wakuu wa vifo hivyo.