"Mamangu anafaa kumchinjia ng'ombe" Akothee afunguka jinsi mkewe Nyong'o alivyomfundisha kuvaa

Akothee alisema anajitahidi kufanana na mama huyo wa muigizaji Lupita Nyong'o.

Muhtasari

•Akothee amekiri kuwa Bi Dorothy Nyong'o ndiye aliyemfanya kuanza kuvaa zinazofunika sehemu kubwa ya mwili wake.

•Akothee alibainisha kuwa mkewe Nyong'o hajawahi kumuuliza sababu za kuchagua mtindo fulani wa mavazi.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuru Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua kuwa mke wa gavana wa Kisumu Anyang' Nyong'o, Bi Dorothy Nyong'o ndiye aliyemfanya kuanza kuvaa zinazofunika sehemu kubwa ya mwili wake.

Wakati alipokuwa akijizolea umaarufu, Akothee alikuwa akipanda jukwaani na kuwaburudisha mashabiki wake huku akiwa amevalia nguo fupi zilizoweka wazi sehemu kubwa ya mwili wake. Hakuwahi kuchukulia hili kama suala kubwa

Mama huyo wa watoto watano amesema siku zote alikuwa mtu wa kuasi hadi alipokutana na Bi Dorothy ambaye alibadili maisha yake kabisa.

"Mtukufu MAMA COUNTY DOROTHY NYONGO. Hajawahi kunihukumu, hajawahi kuniambia nisifanye chochote, amekuwa akiniambia kila mara niwe mimi. Kweli, nimekuwa karibu naye kwa miaka miwili sasa, na tazama kile amefanya. ✔️ Nampenda akiwa amevalia nguo ndefu na umbo lake la kifahari la kutamaniwa , anafanya nguo ndefu zionekane za kupendeza, alinifundisha kuwa sio lazima uonyeshe ngozi ili uonekane mrembo, kifuniko kingine kinavutia pia," Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Alibainisha kuwa mama huyo wa muigizaji maarufu Lupita Nyon'go hajawahi kumuuliza sababu za kuchagua mtindo fulani wa mavazi.

Akothee alisema ingawa hajafanikiwa kabisa kuendana na mtindo wa mavazi wa Bi Dorothy, anajitahidi sana kufanana naye.

"Njia yake ya malezi ilikuwa tofauti, labda alielewa safari yangu, au alitaka kuelewa kwa nini ninajibeba hivyo, sijawahi kuelewa kwa nini yeye haoni aibu na vile watu wanavyofikiri kunihusu mimi. Wakati mwingine nalazimika kujibana ikiwa ni kweli ananikubali kama nilivyo. Ooh ndio, ananikubali. Upendo wake kwangu ni wa kweli, naweza kuuhisi katika mtiririko wa damu yangu, ninamwita wakati ulimwengu wangu unashuka, bila hofu ya hukumu yoyote. Yeye ni Mama na Mshauri," Alisema.

Kufuatia jukumu kubwa alilocheza maishani mwake, Akothee amemsherehekea Bi Dorothy na kumtaja kama mamake wa pili.

"Mama yangu anafaa kumchinjia ng'ombe Mheshimiwa Mama Dorothy Nyong'o kwa kumpinda samaki mkavu. Aliweza kufanya Akothee kuvaa, aliweza kubadili Akothee bila kusema neno," Alisema mwanamuziki huyo.