Mwanaume apata madini ya Ksh 113M baada ya kuchimba migodi kwa miaka 15

Kawishe alilala maskini na kuamka tajiri.

Muhtasari

• Baada ya miaka 15 ya mahangaiko, Ansalem Kawishe alipata madini ya Tanzanite yenye uzito wa kilo 3.74 na 1.4 mtawalia.

• Madini hayo aliyauza kwa serikali ambayo ilimpa shilingi bilioni 2.2 za Tanzania, sawa na milioni 113 pesa za Kenya.

Mchimba migodi alitunukiwa bilioni 2.2 za Tanzania kwa kupata madini ya Tanzanite
ANSALEM JOHN KAWISHE Mchimba migodi alitunukiwa bilioni 2.2 za Tanzania kwa kupata madini ya Tanzanite
Image: Millard Ayo//YouTube screengrab

Kulala maskini, kuamka Tajiri! Ndio hadithi ya mchimba migodi ya madini Ansalem Kawishe kutoka taifa la Tanzania aliyepata mamilioni ya pesa baada ya kuchimba na kupata madini aina ya Tanzanite kwa serikali ya taifa hilo.

Kawishe ambaye alifichua kwamba amekuwa mchimba migodi kwa miaka 15 bila kikomo alikabidhiwa takrima ya shilingi bilioni 2.2 za Tanzania ambazo ni sawa na milioni 113 pesa za Kenya.

Kulingana na jarida la The Citizen la nchini humo ambalo muda mwingi huandika kwa lugha ya Kiingereza, madini hayo moja lilikuwa na uzito wa kilo 3.74 ambalo bei yake ilikuwa bilioni 1.5 za Tanzania sawa na milioni 76.8 za Kenya na la pili lilikuwa na uzito wa kilo 1.4 thamani ya milioni 713.8 za Tanzania sawa na milioni 36.5 za Kenya. Jarida hilo lilimnukuu katibu wa kudumu katika wizara ya madini nchini humo Adolf Nduguru.

Tajiri bilionea huyo mpya kabisa katika udongo wa Tanzania alipewa ulinzi mkali mara moja na kusindikizwa hadi ofisini alipotoa hotuba kuhusu jinsi alianza safari ya uchimbaji madini na jinsi alivyoangukia bahati hiyo ambayo imevusha maisha yake kabisa kutoka upande wa kiza Kwenda nuruni.

“Nimekuwa mpambanaji wa kutafuta Tanzanite zaidi ya miaka 15 iliyopita kupitia migodi ya watu wengine tofauti tofauti,” alisema katika mahojiano na Ayo Tv.

Jarida la The Citizen liliripoti kwamba Waziri wa uchimbaji madini nchini humo Doto Biteko alipomjulisha rais Samia Suluhu kuhusu kupatikana kwa madini hayo, rais aliamuru madini hayo kuuzwa haraka iwezekanavyo na mchimba madini huyo kupewa pesa zake zote bila kukatwa hata senti.