Gidi atamani ingewezekana wanaume kupunguza vitambi kama jinsi Vera alipunguza makalio yake

Mtangazaji Gidi ni miongoni wa waliotoa hisia zao baada ya Vera kufanyiwa upasuaji wa kupunguza makalio.

Muhtasari

•Katika maelezo yake, Vera alisema kuwa maswala ya kiafya yalimfanya afanyiwe upasuaji wa marekebisho.

•Maelfu ya wanamitandao Wakenya walieleza hisia zao kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii

Gidi na Vera Sidika
Image: INSTAGRAM

Mwanasoshalaiti Vera Sidika aliwashangaza wanamitandao wengi siku ya Jumatano alipoonyesha mabadiliko ya mwili wake baada ya kufanyiwa kile alichosema ni upasuaji wa marekebisho.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa binti mmoja ambaye hapo awali alitambuliwa kwa makalio yake makubwa alipakia picha iliyoonyesha yakiwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Katika maelezo yake, Vera alisema kuwa maswala ya kiafya yalimfanya afanyiwe upasuaji wa marekebisho.

"Hii imekuwa awamu ngumu zaidi maishani mwangu, Kwa sababu ya hatari na matatizo ya kiafya, ilinibidi kufanyiwa upasuaji. Bado haiaminiki sana lakini nimekubali na nimejifunza kujipenda bila kujali. Wanawake; tafadhali jifunzeni kujipenda na msiwahi kuruhusu shinikizo la rika likuharakishe katika mambo yatakayowaharibia siku zijazo. Nina bahati ya kuwa hai, Mungu ananipenda sana," alisema.

Mpenzi huyo wa Brown Mauzo alidai kuwa hata hakuweza kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake kutokana na matatizo ya kiafya.

Alisema ingawa mwili wake umebadilika, yeye bado ni Vera yule wa awali na kuwasihi mashabiki wake waendelee kumsapoti.

"Nitakuwa nichapisha video za safari ya upasuaji, kwa wale ambao wamekuwa wakifikiria kupata upasuaji wa makalio au kubadilisha chochote kwenye miili yao hii inaweza kubadilisha mawazo yako," alisema.

Kufuatia hilo, maelfu ya wanamitandao Wakenya walieleza hisia zao kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Mtangazaji wa Gidi na Ghost asubuhi, Joseph Ogidi almaarufu Gidi ni miongoni wa waliotoa hisia zao.

"Natamani sana ingekuwa rahisi kwa sisi wanaume kupunguza tumbo zetu kama jinsi Vera alivyofanyia makalio yake," alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Wanamitandao wengine pia hawakumwacha mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 huku kila aina ya memes zikitumiwa kukejeli muonekano wake mpya.