(+video) Waumini wamenyana katika kanisa la Ng'ang'a katika harakati ya kuondoa mapepo

Waumini hao walionekana kuangushana chini kwa njia ya kivita huku mchungaji Ng'ang'a akiwashabikia kwa furaha.

Muhtasari

• Wengine walionekana kukwaruzana vikali baina ya maombi na kuangushana chini kwenye sakafu ya madhabau.

Mchungaji wa kanisa la Neno, James Ng’ang’a ni mmoja kati ya wachungaji ambao wanajulikana kwa mitikasi yao mitandaoni na pia katika kanisa lake.

Wikendi iliyopita, kioja cha ajabu kilitokea katika kanisa lake ambapo mtafaruku ulitokea kwenye mimbari ya kanisa hilo baada ya kile kiichosemekana kuwa roho mtakatifu kuwaingia baadhi ya waumini.

Katika klipu ambayo imekuwa ikisambazwa mitandaoni, mchungaji Ng’ang’a anaonekana akihubiri na ilipofika zamu ya kufanya maombi ya toba, waumini kadhaa wanasimama kwa ajili ya maombi na kuanza kuonesha ishara za ukichaa.

Wengine walionekana kukwaruzana vikali baina ya maombi na kuangushana chini kwenye sakafu ya madhabau huku wakipukutika chini kwa vishindo na mishe za kivita.

Mchungaji Ng’ang’a alionekana kushabikia tukio hilo huku akiwasihi waumini wengine kutowazuia au kuwakamata wale waliojawa na roho mtakatifu huku akisikika akishabikia kwa maneno kwamba ‘mwache aingie kwenye uwanja!’

Wengi wa waumini hao walioingiwa na nguvu za kiroho walikuwa wanawake na baadae Muda si muda baadhi ya vijana wa kiume pia wakajiunga na kuanza kupigana mieleka kwa taratibu.

Pambano lilionekana kutokuwa na madhara na vitendo vilionekana kuchanganyikiwa. Matukio yalionekana kama yale ya ukumbi wa michezo. Kuelekea mwisho wa klipu hiyo, Ng'ang'a aliomba waumini wote walisifu jina la Yesu Kristo huku akijipangusa kijasho kwa hanchifu kama mtu ambaye ametoka kufanya kazi nzito ya kuondoa mapepo kwa waumini wake.