"Mwili mpya unakuja!" Kinuthia afanyiwa utaratibu wa kubadilisha umbo la mwili

Tiktoker huyo alidokeza kuwa tupo katika siku za mwisho za kumuona na umbo lake la mwili la sasa.

Muhtasari

•Kinuthia aliwatangazia wafuasi watarajie kumuona na mwili mpya na kudokeza anapanga kupitia utaratibu wa kupunguza uzito wa Gastric Ballon.

•"Nafurahia mwili wangu siku chache za mwisho," alisema.

Image: INSTAGRAM// OFFICIAL KINUTHIA

Mtumbuizaji maarufu wa Tiktok Kelvin Kinuthia amedokeza kuhusu mpango wake wa kufanyiwa upasuaji ili kubadilisha umbo lake na kupunguza uzito wa mwili.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kinuthia ambaye anatambulika zaidi kwa kuvalia mavazi ya kike na ya kiume aliwatangazia wafuasi wake watarajie kumuona na mwili mpya na kudokeza anapanga kupitia utaratibu wa kupunguza uzito wa Gastric Ballon.

"Usiogope kushindwa. Ogopa kuwa mahali sawa mwaka ujao kama ulivyo leo. Mwili mpya unakuja.." alisema siku ya Ijumaa.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha iliyomuonyesha akiwa katika kituo kimoja cha kufanya mchakato wa gastric ballon.

"Malengo mapya ya mwili," aliongeza.

Katika chapisho lao la shukrani kwa Kinuthia kwa kuwachagua, kituo hicho kilidokeza kuwa mtumbuizaji huyo tayari alikuwa ameanza mchakato wa kupunguza uzito.

"Asante kwa kutuamini kwa mabadiliko yako mpendwa.. tufanye hili, tumefurahi kwa ajili yako," kituo hicho kilisema kupitia Instagram.

Jumamosi asubuhi Kinuthia alipakia video iliyomuonyesha akicheza densi ndani ya nyumba yake. Chini ya video hiyo alidokeza kuwa tupo katika siku za mwisho za kumuona na umbo lake la mwili la sasa.

"Nafurahia mwili wangu siku chache za mwisho," aliandika.

Uwekaji wa puto ndani ya tumbo (gastric ballon) ni utaratibu wa kupunguza uzito unaohusisha kuweka puto ya silikoni iliyojaa chumvi kwenye tumbo. Puto hizo  husaidia kupunguza uzito kwa kuongeza shibe, kuchelewesha utoaji wa juisi ya tumbo na kupunguza kiwango cha chakula kinacholiwa katika kila mlo.

Siku za hivi majuzi watu wengi wakiwemo wasanii maarufu wamekuwa wakipitia taratibu hiyo katika juhudi za kupunguza uzito.

Mtangazaji wa Citizen TV Willis Raburu, muigizaji Catherine Kamau almaarufu Cate Actress, mwanamuziki  Big Ted, Murugi Munyi, mwanasoshalaiti Risper Faith na muigizaji wa Bongo Wema Sepetu ni miongoni mwa wasanii ambao wamefanyiwa taratibu ya gastric bypass katika siku za hivi majuzi.