Bahati na Diana wafichua jinsia ya mwanao katika hafla ya kifahari

Marua alifichua jinsia ya mwanawe mtarajiwa kwa sherehe iliyoandaliwa na mume wake, Bahati

Muhtasari

• Marua alisema kuwa hakuwa ametarajia kumpokea mtoto wa kike, alikuwa ametarajia mtoto wa kiume kwa alivyokuwa anahisi.

Bahati na Diana Marua

Mwanamuziki Bahati alimwandalia mkewe Diana Marua sherehe ya kufichua jinsia ya mtoto mtarajia.

Bahati alimwambia mkewe kuwa alikuwa anampeleka mahali pa kujivinjari ili wale chamcha ama chajio kama njia ya kumshukuru kwa safari hiyo aliyopitia.

Mwanamuziki huyo aliwaalika marafiki wa Marua kwenye hafla hiyo ili waweze kusherehekea naye hatua hiyo kubwa.

Kulingana na sherehe hiyo, ilifichuka kuwa wanandoa hao wanatarajia mtoto wa kike, jambo ambalo lilimpa mkewe Bahati machozi ya furaha.

"Nina furaha sana. Sina maneno. Wakati huu wote nimekuwa nikijua kuwa namtarajia mtoto wa kiume, kwa sababu ya alivyokuwa anageuka. Nilikuwa natumai kupata mtoto wa kiume baada ya hapo na nilikuwa tayari," Marua alisema akijizuia kulia.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa pia yeye alikuwa anamtarajia mtoto wa kiume na kuufananisha na siasa zake alipokosa kushinda kwenye uchaguzi wa Agosti.

Bahati alisema kuwa yuko tayari kumkaribisha binti yake na kueleza furaha aliyokuwa nayo licha ya kupata mtoto wa kike ambaye hakuwa ametarajia.

Alimwandikia mkewe ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram na kumshukuru kwa kumbeba mwanawe kwa unyenyekevu kwa miezi tisa.

"Ninakupenda sana mpenzi wangu," Bahati alimwandikia Marua

Mama huyo wa watoto wawili alimwandikia mwanawe mtarajiwa ujumbe ulioonyesha anavyomsubiria.

Marua alisema kuwa safari hiyo yake ya uja uzito haijakuwa nzuri vile ila ilimsaidia kuwa na uhusiano wa karibu na mtoto wake.

Kulingana na video aliyopakia Jumanne asubuhi katika ukurasa wake wa Instagram, Marua alionekana kuwa mchangamfu mno.

Alisema kuwa amesubiria sana kufichua jinsia ya mtoto wake na kuwa hata yeye amekuwa na furaha kusubiria hilo.