Inahuzunisha sana!Kambua amfariji Davido baada ya kumpoteza mwanawe

Muhtasari
  • Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto wawili alieleza kifo cha mtoto kuwa cha kusikitisha na kuhuzunisha
Mwinjilisti Kambua
Mwinjilisti Kambua
Image: INSTAGRAM

Watu maarufu mbali mbali walijumuika na msanii Davido kuomboleza kifo cha mtoto wake wa kiume huku mitandao ikijaa uvumi na maneno mengine ya kustaajabisha.

Mwimbaji Kambua ameandika ujumbe wa hisia kwa mwimbaji wa Nigeria Davido baada ya kumpoteza mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto wawili alieleza kifo cha mtoto kuwa cha kusikitisha na kuhuzunisha.

Aliendelea kuomba Mungu amfariji mwimbaji huyo na mkewe.

"Kifo cha mtoto si cha kawaida. Inasikitisha. Inahuzunisha sana. Mungu amfariji David na mkewe. Wiki chache zilizopita nilisema- majeneza madogo ndio mazito zaidi. Mungu wa faraja yote awe karibu nao," aliandika. .

Mtoto wa Davido na mpenziwe Chioma Rowland, Ifeanyi anaripotiwa kufariki Jumatatu usiku baada ya kuzama kwenye kidimbwi cha kuogelea.

Kulingana na ripoti, Ifeanyi ambaye hivi majuzi alitimiza umri wa miaka mitatu alikuwa akiogelea kwenye kidimbwi kilicho nyumbani kwao katika eneo la Kisiwa cha Banana, Jimbo la Lagos, Nigeria alipokufa maji.

Inaripotiwa kwamba mvulana huyo mdogo alikaa chini ya maji kwa muda mrefu kabla ya hatimaye kuonekana na kukimbizwa katika hospitali ya Lagoon iliyo eneo la Ikoyi ambako alithibitishwa kufariki.

Davido na mpenziwe Chioma walikuwa wamesafiri hadi Ibadan kwa mkutano wa familia na walikuwa wamemwacha Ifeanyi na walezi wake ambao hawajaweza kueleza jinsi alivyoingia kwenye bwawa hilo bila kutambuliwa na hatimaye kuzama.