Mwandani wa Diamond, Baba Levo, azungumza baada ya kudaiwa kufariki katika ajali ya ndege

"Bongo movie naomba tuheshimiane, msiniue!!" Baba Levo alisema.

Muhtasari

•Video ya ajali hiyo yenye maandishi ‘RIP Baba Levo’ ​​ilitengezwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

•Watu 19 walifariki katika ajali hiyo na wengine 26 kuokolewa.

Image: INSTAGRAM// BABA LEVO

Mwimbaji wa Bongo mkongwe Baba Levo amejitokeza kuzika tetesi kuwa alikuwa miongoni mwa watu walioangamia katika ajali ya ndege iliyotokea katika eneo la Bukoba, mkoa wa Kagera siku ya  Jumapili.

 Jumapili asubuhi, ndege ya shirika la Precision Air ambayo ilikuwa ikitoka jijini Dar es Salaam kuelekea Bukoba kupitia Mwanza ilianguka na kuzama karibu na ufuo wa ziwa Victoria, upande wa Tanzania.

Watu 19 walifariki katika ajali hiyo na wengine 26 kuokolewa.

Madai kuwa Baba Levo ni miongoni mwa waliofariki kwenye ajali hiyo yaliibuka baada ya video yake akipanda ndege ya Precision Air, sawa na iliyihusika kwenye ajali kusambaa mitandaoni. Mwimbaji huyo alikuwa amepakia video hiyo kwenye akaunti yake ya Instagram Jumapili Asubuhi kabla ya habari za ajali kuvuma.

Tayari watu walikuwa wameanza kuhoji hatma ya mwandani huyo wa Diamond Platnumz wakati video ya ajali hiyo yenye maandishi ‘RIP Baba Levo’ ​​ilipotengezwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

"Bongo movie naomba tuheshimiane, msiniue!!" Baba Levo alijibu madai ya video hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mamia ya mashabiki wa mwimbaji huyo walieleza kufarijika kwao baada ya kufahamu kuwa bado  yuko hai.

Wasanii maarufu wa Bongo akiwemo Diamond, Harmonize na Alikiba walituma salamu zao za rambirambi kufuatia ajali hiyo ya Jumapili.

Kwenye kurasa zao, Harmonize na Diamond walipakia picha ya mshumaa na njiwa kuashiria wanaomboleza waliofariki. Alikiba kwa upande wake aliwafariji wanafamilia wa walioaga na kuwatakia afueni majeruhi wote.

"Mwenyezi Mungu azilaze roho  za wapendwa tuliowapoteza mahala pema na awatie faraja ndugu na jamaa waliopoteza ndugu na jamaa zao. Tunawaombea majeruhi wote kwa mwenyezi Mungu awape Nguvu na kuwarejeshea utimamu wa afya zao," sehemu ya taarifa ya Kings Music Records ilisoma.

Rais Samia pia alituma salamu za pole kwa waathiriwa wa ajali hiyo na kuwashukuru wakazi wa Kagera kwa ujasiri, ushirikiano na jitihada walizofanya kuwaokoa abiria waliozama na ndege hiyo.